Barabara ya juu katika eneo la Tazara ambayo inazinduliwa leo na Rais Dkt.John Pombe Magufuli ujenzi wake umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 100.52 na umejengwa kwa ushirikiano wa serikali ya Japan kupitia shirika lao la msaada la JICA.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Magufuli ameigiza TANROAD kufunga CCTV cameta mara moja katika maeneo yote ya Daraja hilo ili kuimarisha ulinzi na kurekodi matukio yote yanayoweza kutokea katika eneo hilo.
Awali, Magufuli alitoa pole kwa familia zilizoondokewa na wapendwa wao kufuatia ajali ya MV Nyerere iliyotokea Septemba 20 mwaka huu huko Ukerewe, Mwanza na kuwaombea majeruhi uponyaji wa haraka huku akiwashukuru Watanzania kwa mshikamano walioonyesha na kusema tukio hilo liwe funzo kwa wahusika.
Aidha, Magufuli amebainisha kuwa Serikali inajenga barabara ya njia 6 kutoka Kimara kwenda Kibaha kwa Sh. Bilioni 140 na fedha zote zinatolewa na Serikali ya Tanzania, pia na njia ndogo 2 (service road) huku akiongeza kwamba ujenzi wa Flyover ya Ubungo itagharimu Bilioni 247.
“Itakuwa flyover ya aina yake kwa Dar es Salaam kwani itakuwa na ghorofa na kutaka flyover ya Gerezani ifanyiwe kazi ambayo tayari hadi tenda yake imeshatangazwa. Nawaomba Japan pia waikumbuke barabara ya Morocco – Mwenge waliyoahidi, imechukua muda mrefu” amesema Magufuli.