Rais Museveni: Wapinzani ni Magaidi na Wahuni

Museveni: Wapinzani ni Magaidi na Wahuni
Rais Yoweri Museveni amewapiga chapa wafuasi wa upinzani kuwa ni “magaidi” na “wahuni” akisema walirushia “mawe” gari lake Agosti 13 hali iliyozua tafrani baada ya kampeni kali za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arua.

Akijibu barua aliyoandikiwa na Spika wa Bunge Rebecca Kadaga, Rais Museveni amesema wafuasi wa Mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine walishambulia gari alilokuwa amepanda kutoka eneo la kampeni akielekea uwanjani kupanda helikopta, na walilirushia mawe siku ile ya Agosti 13.

“Ilikuwa muda mfupi baada ya kupita tingatinga nikasikia milio miwili kwenye gari langu. Niliarifiwa baadaye na ADC wangu kwamba gari langu lilipigwa mawe yaliyorushwa na makundi ya upinzani yaliyokuwa yakiandamana. Nilishauri msafara wangu kuwapuuza wale wahuni na tukaelekea kupanda helikopta jambo walilofanya bila kurusha risasi yoyote,” inasema sehemu ya barua ya Museveni iliyoandikwa Agosti 31.
Maelezo haya ya Rais kwa Spika yanakinzana na mengine aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii ambapo alisema gari la kubeba mizigo katika msafara wake ndilo lililopigwa mawe katika siku ile ya mkasa.

Taarifa ya awali
Katika taarifa aliyoitoa mwezi uliopita Museveni alisema: “Mawe waliyorusha yalivunja kioo cha nyuma cha gari linalobeba mizigo. Kioo cha dirisha lile hakijaundwa kuzuia risasi kupenya. Hakukuwa na madhara yoyote kwa yule mzee anayevaa kofia.”
Alisema alitaka kumtaafiru Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) lakini badala yake alimtaarifu Kamanda wa Brigedi kwa sababu RPC hakuwepo katika Shule ya Msingi ya Pokea ambako alipanda helikopta Arua.
“Mara baada ya kuondoka SFC (askari wa kikosi maalumu cha kumlinda rais) walirudi mjini kuwasaidia polisi kutawanya kundi la watu ambalo kwa uwazi lilikuwa limeshindwa kujidhibiti kwani hawakuona tatizo kurushia mawe gari la Rais wa Uganda,” aliandika Rais.
Pia alidai kwamba wafuasi wa Kyagulanyi walikuwa wamekodi “tingatinga, labda kwa ajili ya kufunga barabara niliyotumia kwenda kwenye uelekeo wangu” na alisema upinzani unasafirisha “magaidi” kutoka Kampala kwenda majimbo mengine.

“Yakiwa sehemu ya madai (kortini), ilielezwa kwamba magaidi wanasafirishwa kutoka maeneo ya Kampala kwenda majimbo ya bara kupiga, kujeruhi na kutisha wapigakura ikiwa ni pamoja na kuharibu mali za raia wetu. Hata kule Rukungiri, kulikuwa na vitisho vya mdomo, watu kushambuliwa na mali kuharibiwa,” alisema Museveni.

Museveni pia amemwambia Spika kwamba ni “makosa na mapema mno kusema kuwa hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya wakosaji ndani ya vikosi vya usalama” kwa sababu Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi (CDF), Jenerali David Muhoozi, na Inspekta Jenerali wa Polisi Martin Okoth-Ochola wameunda kamati za kuchunguza maofisa waliopotoka.”
Pia Museveni amemwambia Spika “ajizuie kutumia neno mateso” hadi uchunguzi wa CDF na IGP utakapokamilika.

Katika hatua nyingine, Naibu Spika Jacob Oulanyah alikataa kuwasomea wabunge barua ya Museveni akisisitiza kwamba “Naibu Spika si msomaji wa barua za Spika.”
Wiki iliyopita, Oulanyah alilazimika kuahirisha Bunge baada ya wabunge kusisitiza kwamba mjadala wa maana kuhusu kilichochochea vurugu katika Manispaa ya Arua lazima uwe na mwongozo wa majibu ya Museveni kwa barua iliyoandikwa na Kadaga Agosti 27.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad