Nyota wa klabu ya Juventus na timu ya taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo, amefunga mabao mawili kwenye mechi ya ligi kuu ya soka nchini Italia ikiwa ni mabao yake ya kwanza kwenye mechi 4 alizoichezea Juventus.
Cristiano Ronaldo amefunga mabao hayo katika dakika za 50 na 65, hivyo kuipa ushindi timu yake ya Juventus wa mabao 2-1 dhidi ya Sassuolo, ambao bao lao limefungwa na Khouma Babacar dakika ya 90.
Baada ya kufunga mabao hayo mawili, Ronaldo sasa amefikisha mabao 400 kwenye ligi tu akifunga katika klabu 4 na ligi 4 tofauti alizocheza mpaka sasa.
Ronaldo aliifungia mabao matatu Sporting CP kwenye ligi ya Ureno kabla ya kufunga mabao 84 akiwa na Manchester United kwenye ligi kuu ya Uingereza, kisha akafunga mabao 311 kwenye ligi kuu ya Hispania akiwa na Real Madrid na leo amefunga mabao mawili kwenye Serie A akiwa na Juventus.
Ronaldo sasa amekuwa mchezaji wa tano kufikisha idadi hiyo ya mabao kwenye ligi pekee, akiwa nyuma ya Josef Bican, Ferenc Puskás, Jimmy McGrory na Uwe Seeler ambao walifikisha idadi hiyo ya mabao kwa nyakati tofauti.