Sakata la Tundu Lissu Laibuka Tena Bungeni....Serikali Yawatupia Lawama CHADEMA

Sakata la Tundu Lissu Laibuka Tena Bungeni....Serikali Yawatupia Lawama CHADEMA
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndio wanachelewesha kukamilika kwa ripoti ya uchunguzi dhidi ya shambulio la mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.

Waziri Masauni ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali laMbunge wa Ubungo (CHADEMA) Saed Kubenea bungeni leo Septemba 14, ambalo lilihoji kuwa kumekuwa na matukio mengi ya kihalifu yanatokea ikiwemo kupotea na kutekwa watu, lakini serikali imekuwa ikionesha kuwalinda zaidi watu wao wa karibu na sio wanaharakati wanaoipinga serikali na kuhoji ni lini ripoti ya serikali itakamilika kuhusiana na tukio la kushambuliwa kwa mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.

Masauni amemtaka Kubenea kufuta kauli yake aliyodai kuwa ni upotoshaji kwa jamii kwani hakuna matabaka katika ulinzi wa raia na mali zao na kusema kuwa;  “Napenda kujibu swali la Kubenea lakini ningependa kumpinga na kumkosoa vikali kwa kauli yake, kwani hakuna matabaka katika kulinda na kusimamia usalama wa raia na mali zao wote na hakuna matabaka, kuhusu shambulio la Tundu Lissu chama chao hakitoi ushirikiano ikiwemo kumficha dereva ambaye ndiye shuhuda namba moja”.

Aidha Masauni ameongeza kuwa masuala ya kigaidi yanahitaji muda zaidi kukamilisha uchunguzi wake kwakuwa huhusisha taasisi nyingine za nje zaidi ya Jeshi la polisi hivyo unahitaji muda na umakini wa hali ya juu.

Suala la watu wasiojulikana limekuwa likiibua mvutano bungeni kila ifikapo zamu ya kuchangia kwa wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi baada ya kuibuka kwa matukio ya utekaji na kupotea kwa watu maarufu kuanzia mwaka 2017 wakiwemo wanahabari na wasanii wa muziki.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad