Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imejipanga kuhakikisha inaipa nguvu, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), ili kuweza kuongeza ubora wa barabara nchini.
Hilo limebainishwa leo na Naibu waziri wa Ujenzi, Mhandisi Edwin Ambandusi Ngonyani, kwenye mahojiano na kipindi cha East Africa Drive, kinachoruka kupitia East Africa Radio kuhusu uwepo wa barabara nyingi mbovu zilizo chini ya TARURA.
''TARURA wamefanyakazi kubwa ya kutambua barabara zipi zinahitaji Lami na zipi zinahitaji Changarawe na baada ya hapo ndipo tunakwenda kuwapa fedha kwaajili ya utekelezaji na tutashuhudia inafanyakazi kama TANROADS'', amesema Ngonyani.
Aidha ameeleza kuwa TARURA imetekeleza shughuli zake kwa mwaka mmoja hivyo ni muda mfupi kusema kazi zake mbovu, lakini serikali inaendelea kuajiri wahandisi ambao watakwenda kufanya kazi huko.
Ameongeza kuwa TARURA wameshautambua mtandao wa barabara nchini ambapo barabara zenye urefu wa kilometa 108,000 watazifanyia tathmini na kuzifanyia kazi ikiwemo kuweka Lami na Changarawe kwa zenye mahitaji hayo.