Katika marekebisho hayo ya sheria, DPP atakuwa na mamlaka ya kuwasilisha mahakamani maombi ya kukamata mali iliyopatikana kwa njia ya uhalifu au isivyo halali pamoja na kumwezesha kuitaifisha au kuiuza.
Sheria hiyo pia inatamka kuwa DPP atalazimika kuiuza mali ya mtuhumiwa ambayo iko hatarini kupotea, kuharibika au utunzaji wake una gharama kubwa kwa serikali.
Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Paramagamba Kabudi, wakati akiwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba mbili wa mwaka 2018.
"Sehemu ya 13 inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Urejeshwaji wa Mali zitokanazo na Uhalifu sura ya 256. Marekebisho yanayopendekezwa yanalenga kuimarisha mfumo wa kisheria kwa kuhakikisha kuwa wahalifu hawafaidiki kutokana na mali walizozipata kwa njia za uhalifu," alisema Prof. Kabudi.
Alisema hatua ya upitishwaji wa sheria hiyo itawezesha kuzuia uhalifu nchini kwa kuwa watuhumiwa wataona kuwa uhalifu haulipi.
"Muswada unapendekeza pia kufanya marekebisho katika kifungu cha 32 cha sheria hiyo kwa lengo la kuwezesha mali zilizopatikana isivyo halali kurejeshwa bila kucheleweshwa," alisema Prof. Kabudi
Aidha, Prof Kabudi alisema sehemu hiyo inapendekeza kuongeza vifungu vya 38A, 38B, 38C kwa lengo la kupokea maelezo na uthibitisho wa nyaraka na viapo.
Prof. Kabudi alisema kifungu cha tatu cha sheria hiyo nacho kitarekebishwa kwa kuboresha tafsiri ya maneno 'Serious Offence' ili pia itumike kwa makosa mengine yote makubwa yanayozalisha kipato.
Alisema tafsiri ya sasa haijumuishi makosa yote ya jinai ambayo yanaweza kusababisha faida kama vile makosa yahusuyo wanyamapori na makosa ya kodi.
Alisema Sheria hiyo pia itafanya marekebisho ya vifungu na kuongeza vifungu vipya vya 31A,31B,31C, ambavyo vinaweka masharti kuhusu kuzuia akaunti ya benki, ukusanyaji wa taarifa au nyaraka kuhusu mali na utoaji wa taarifa za kiuchunguzi.
Alisema lengo la marekebisho hayo ni kuviwezesha vyombo vya uchunguzi kupata taarifa inayoweza kusaidia katika uchunguzi na kuzuia utoaji wa taarifa ambazo zinaweza kuathiri uchunguzi wa mali itokanayo na uhalifu.
Alisema kutokana na mabadiliko hayo, DDP ataweza kuwasilisha maombi ya upande mmoja ya kukamata mali inayopatikana kwa njia ya uhalifu na ambayo iko hatarini kupotea au kuharibika.
Wakichangia kuhusu kifungu hicho, Mbunge wa Songea Mjini (CCM), Dk. Damas Ndumbalo, alisema kama watu wanachuma mali kwa njia isiyo halali ni vyema sheria ichukue mkondo wake.
"Sheria hii siyo ngeni imekuwa ikitumika nchi mbalimbali, kama mtu unapata mali kwa njia ya uhalifu wacha tu sheria ichukue mkondo wake, na mali zinazozungumziwa ni magari, nyumba na vinginevyo," alisema Dk. Ndumbalo.
Naye Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Emmauel Mwakasaka, alitoa tahadhari kwa Serikali kwa kueleza kuwa sheria hiyo itakapoanza kutumika itende haki na isitumike kwa chuki na kuwakomoa watu.
Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea, alisema kukamata mali za mtuhumiwa na kuziuza siyo sawa kwani itaathiri familia ya mtuhumiwa.
Akitolea ufafauzi wa suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Adelardus Kilangi, alisema kazi ya ukamataji mali litahusisha mali zisizoweza kutoroshwa au kuharibika na fedha zitakazopatikana zitahifadhiwa katika akaunti maalum hadi pale kesi itakapomalizika.