Serikali ya Tanzania imesema itapinga mipango ya serikali ya Kenya kujenga mabwawa ya kuzalisha umeme na kilimo cha umwagiliaji kwenye Mto Mara.
Kwamujibu wa waziri wa mazingira wa Tanzania, January Makamba iwapo mipango hiyo ya Kenya itatekelezwa, itapunguza mtiririko wa maji na kutishia ustawi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mto Mara unaanzia nchini Kenya kwenye milima ya Mau na kutiririka mpaka Tanzania ambako unatengeneza sehemu ya mpaka wa nchi hizo mbili. Mto Mara pia unatenganisha Hifadhi za Taifa za Masai Mara ya Kenya na Serengeti ya Tanzania.
Ni katika Mto Mara pia ambapo Nyumbu huvuka kwa wingi kutoka upande wa Tanzania kwenda Kenya na kuvutia maelfu ya watalii kwenye mbuga za Serengeti na Masai Mara kushuhudia tukio hilo ambalo linatajwa kama moja ya kivutio cha asili cha dunia.