Serikali Yamnyima Kibali cha Kazi Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Vodacom

Serikali Yamnyima Kibali cha Kazi Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Vodacom
Serikali imetangaza rasmi kumnyima kibali cha kazi Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Kampuni ya Simu za mikononi ya Vodacom, raia wa Kenya, Sylvia Mulinge.

Kampuni ya Vodacom ilisambaza ujumbe jana ikisema sasa ni rasmi kuwa mkurugenzi huyo hawezi kupewa kibali cha kufanya kazi nchini.

"Vodacom Tanzania inathibitisha kuwa serikali ya Tanzania imekataa kutoa kibali cha kazi kwa Sylvia Mulinge na sasa itaanza mchakato wa kumpata mkurugenzi mpya," ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ambayo ilitolewa na Mwenyekiti wa Vodacom Tanzania, Ali Mufuruki, ilisema wamekatishwa tamaa na kusikitishwa na uamuzi wa Kamshina wa Kazi na wamejipanga kuwasiliana na mamlaka.

"Tunauhakika kwamba Vodacom ina timu imara ya usimamizi ambayo itaiongoza kampuni vyema mpaka pale suala la kutafuta kiongozi mwingine anayefaa litakapomalizika," ilieleza taarifa hiyo.

Mulinge ambaye anaongoza idara ya biashara kwa wateja katika kampuni ya simu ya Safaricom ya Kenya, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Aprili, mwaka huu.

Hata hivyo, alishindwa kuanza kazi katika kipindi alichoteuliwa kutokana na kusubiri kupata kibali cha kufanya kazi Tanzania.

Wakati akisubiri kibali hicho, Vodocom imetoa taarifa ikieleza kunyimwa kibali cha kazi kwa mkurugenzi mpya ambaye alitakiwa kuanza rasmi majukumu yake tangu Juni mwaka huu.

Aidha, Kampuni ya Vodacom Tanzania ilimteua Hisham Hendi, kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji kuanzia Septemba 1, mwaka huu, mpaka mchakato wa kumpata mkurugenzi mtendaji mpya utakapokamilika.

Hendi amekuwa na kampuni ya Vodacom Tanzania tangu mwaka 2016 akiwa Mkurugenzi wa Biashara. Pia ana uzoefu wa miaka 15 katika sekta ya mawasiliano na amewahi kushika nafasi mbalimbali katika kampuni ya Vodafone na kampuni mama ya Vodacom Group.

Uteuzi huo wa Hendi umefanyika ikiwa imepita miezi minne tangu Mulinge alipotakiwa kuchukua nafasi ya aliyekuwa akishika nafasi hiyo, Ian Ferrao, ambaye pia alikosa kibali cha kufanya kazi nchini.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad