Serikali kupitia Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imenunua mashine mbili mpya za kisasa zenye thamani ya shilingi bilioni 9.56 kwa ajili ya kutoa tiba ya mionzi kwa wagonjwa wa Saratani hapa nchini.
Hayo yamebainishwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati akizungumzia kuhusu utekelezaji wa wizara hiyo katika kipindi cha Tunatekeleza kilichorushwa na kituo cha Televisheni cha TBC.
“Mashine hizi za kisasa zimeboresha utoaji wa tiba ya mionzi hasa kupunguza muda kutoka wiki 6 hadi wiki 2 kwa mgonjwa mpya wa Saratani ambaye anapaswa kuanza tiba hiyo,” alisema Ummy.
Aidha alieleza kuwa hali ya upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa wa Saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imeimarika sana kutoka asilimia 4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 85 mwezi Julai mwaka huu.
Katika hatua nyingine Ummy alisema kuwa Serikali imeboresha huduma za hospitali za rufaa za kanda kwa kufungua majengo mapya na kufunga mashine za mionzi ya tiba ya Saratani katika hospitali za KCMC mjini Moshi, Bugando Jijini Mwanza na Hospitali ya Rufaa ya Mbeya hatua ambayo itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa dawa muhimu kwa ujumla katika maeneo yote hapa nchini, Ummy alieleza kuwa katika vituo vya kutolea huduma za afya upatikanaji wa dawa umeimarika hadi kufikia asilimia 89.6 kutoka asilimia 35 mwaka 2015.
Alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeongeza kwa kiasi kikubwa bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 iliyokuwepo mwaka 2015/2016 hadi kufikia bilioni 270 mwaka 2018/2019.
“Katika kuhakikisha dawa hizo zinafika kwenye maeneo yote, Serikali imenunua magari 181 kwa ajili ya kusambaza dawa na hivi sasa dawa zinapelekwa moja kwa moja kwenye kituo cha afya badala ya kupelekwa kwenye makao makuu ya halmashauri kama ilivyokuwa awali,” alisisitiza Ummy.
Pia alisema kuwa Serikali imeimarisha huduma za matibabu ya kibingwa kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na hivyo kupunguza rufaa za wagonjwa nje ya nchi kutoka wagonjwa 553 mwaka 2015 mpaka kufikia wagonjwa 103 mwaka 2018.
Alisisitiza kuwa hatua hiyo imewezesha wananchi wengi kupata huduma za kibingwa ndani ya nchi na pia kuokoa fedha nyingi za Serikali.