Serikali Yapigilia Msumari Makato ya Asilimia 15, Kwenye Mishahara ya Wanufaika wa Mikopo ya Elimu ya Juu

Serikali yapigilia msumari makato ya asilimia 15, kwenye mishahara ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu
Serikali imeweka bayana kuwa haina mpango wowote wa kufuta makato ya asilimia 15, kwenye mishahara ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu nchini na itachukua hatua kali kwa wale wanaochelewesha kulipa fedha hizo wakati wapo kazini.

Hilo limebainishwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof. Joyce Ndalichako leo Sep, 12, 2018 bungeni, wakati akijibu swali la mbunge wa Mbozi Pascal Haonga lililohoji juu ya ongezeko la makato ya wanufaika wa mikopo kutoka asilimia 8 hadi 15.

Katika swali hilo Haonga alitaka kujua kwanini serikali isiingilie kati suala la kupandishwa kwa makato hayo na bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ili kunusuru wafanyakazi ambao wanalalamika kukosa nauli za kwenda kazini kutokana na makato hayo kuwa makubwa.

Prof. Ndalichako amesema Serikali itaendelea kukata makato hayo kwani taratibu zote za kupandishwa kwa asilimia zilifuatwa, ikiwemo kuwashirikisha wadau ambao ni wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi TUGHE na TUCTA, Chama cha Mawakili (TLS) pamoja na wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini.

"Makato ya asilimia 15 ya mishahara ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu yamewekwa kisheria kwa lengo la kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali zinarejeshwa kwa wakati kwa lengo la kusaidia wengine hivyo serikali haina mpango wa kupunguza au kusitisha makato hayo,'' amesema.

Aidha, Prof. Ndalichako ametoa wito kwa wanufaika wa mikopo hiyo kuhakikisha wanajisajili na kuanza kurejesha mikopo hiyo mara tu waingiapo kwenye ajira na wanaokiuka kufanya hivyo wataendelea kushughulikiwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad