Serikali imesitisha uagizwaji wa mchele kutoka nje ya nchi kutokana na uliopo nchini kutosheleza mahitaji.
Mchele uliopo nchini kwa sasa ni zaidi ya tani milioni 2.2, kiwango kilichotokana na wakulima wa mpunga kupatiwa mbinu bora za kitaalamu.
Katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mathew Mtigumwe alisema jana kuwa mahitaji ya mchele yanatosheleza kwa sasa.
Mtigumwe alisema hayo wakati akizungumza na wakulima wa mpunga kutoka mikoa mbalimbali nchini katika mafunzo yaliyofanyika mjini Moshi yaliyofadhiliwa na Shirika la Misaada la Japan (Jica).
Alisema mahitaji ya mchele nchini ni tani 900,000 na kwamba uzalishaji kwa sasa umeongezeka na nchi ina ziada ya zaidi ya tani milioni 1.2.
“Serikali mwaka huu haina haja ya kuagiza mchele kutoka nje ya nchi, ” alisema Mtigumwe
Alisema wanatambua mchango wa kuwasaidia wakulima unaofanywa na Jica ambapo wale wadogo wa mpunga wamefanikiwa kuongeza kiwango cha uzalishaji tofauti na siku za nyuma.
“Kutokana na uzalishaji huu umeifanya Tanzania kuwa nchi ya tano Kusini mwa Jangwa la Sahara katika uzalishaji wa mpunga baada ya nchi ya Nigeria, Madagascar, Mali na Guinea.”
Mwakilishi mkuu wa Jica nchini, Toshio Nagase alisema zaidi ya wakulima 15,000 wamenufaika na mradi huo na kuweza kujikwamua na umaskini.
Serikali Yasitisha Uagizwaji wa Mchele Nje ya Nchi
0
September 14, 2018
Tags