Serikali Yatoa Ufafanuzi Gonjwa Jipya Laibuka

Serikali Yatoa Ufafanuzi Gonjwa Jipya Laibuka
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema, mpaka sasa haijafahamika kinachosababisha ugonjwa wa Lupa, ambao umeua mtu mmoja huku 10 wakiwa wanafuatiliwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile, jana Septemba 06, 2018 Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 03 mkutano wa 12 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu swali la la Mbunge, Asha Jecha, aliyetaka kufahamu chanzo cha ugonjwa wa Lupa pamoja na idadi ya watu walioguwa na kufariki nchini.

"Hadi sasa watafiti hawajaweza kujua chanzo cha ugonjwa wa Lupa, inasadikiwa mgonjwa mwenye vinasaba vya Lupa, hupata ugonjwa huo pale anapopatwa na visababishi kwenye mazingira yanayochochea kupata maradhi hayo. Vitu vinavyochangia kupata ugonjwa huo ni miale ya jua, maambukizi ya bakteria, matumizi baadhi ya dawa ya shinikizo la damu, dawa za kifafa na 'antibiotic", alisema Dkt. Ndugulile na kuongeza;

"Ugonjwa wa Lupa ni ugonjwa wa kinga za mwili ambao hushambulia viungo vya mwili vikidhania kwamba ni vitu vigeni. Viungo ambavyo hudhurika zaidi ni ngozi, figo, ubongo, chembe chembe za damu, moyo, mapafu na viungo vingine vya mwili kama 'joint".

Aidha, Dkt. Ndugulile alisema ugonjwa huo huwapata zaidi watu wenye jinsia ya kike (wanawake)  wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi kufikia 45.

"Ugonjwa huu hauna tiba bali hutolewa dawa za kupunguza athari tu, katika hospitali ya Muhimbili hugundulika watu wenye ugonjwa huu wawili kwa kila mwaka na hupatiwa tiba kwenye kliniki ya ngozi, na hadi hivi sasa kuna wagonjwa takribani 10 wanaofuatiliwa", alisisitiza Dkt. Faustine.

Kwa upande mwingine, serikali imesema imejipanga kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwamo kutekeleza mkakati wa nne wa taifa wa kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2018 hadi 2023, ili kumaliza au kutokomeza kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030 kama ilivyoadhimiwa na Umoja wa Mataifa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad