Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro imepiga marufuku wanafunzi kuhudhuria sherehe ya aina yeyote ile zaidi ya saa 12 jioni, lengo likiwa ni kupunguza mimba za utotoni baada ya kukithiri kwa kesi za ujauzito kwa wanafunzi.
Akizungumza na wadau wa elimu katika kikao cha kujadili namna ya kumlinda mtoto wa kike, Afisa Takwimu Idara ya Elimu Sekondari, Salome Msegeya amesema kuwa wazazi wamekuwa chanzo cha watoto wa kike kujiingiza kwenye hivyo kupiga marufuku mwanafunzi kuhudhuria sherehe inayoanza mida ya kuanzia saa 1 usiku na kuendelea.
“Wanafunzi wamekuwa wakitumia sherehe hizo kuanzisha mahusiano yanayopelekea kupata ujauzito Halmashauri imeamua kujidhatiti kutokomeza tatizo hilo”, amesema Afisa Takwimu.
Kwa upande wake Mratibu wa Dawati la Polisi la jinsia wilaya ya Hai Happiness Eliufo amesema kuwa jamii hiyo bado inahitaji elimu zaidi ili kuokoa watoto wa kike kwani matukio yamekuwa mengi huku watuhumiwa wakifichwa.
Wanafunzi 26 katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wamesitisha masomo yao katika kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba 2018, baada ya kupata ujauzito, huku 11 kati yao wakiwa ni wanafunzi wa kidato cha nne.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto, (Unicef) kati ya mwaka 2010 na 2017, Tanzania ni ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa na mimba za utotoni baada ya Sudan Kusini na Uganda.