KIUNGO wa Simba Mnyarwanda, Haruna Niyonzima anatarajia kukumbwa na adhabu ya kukatwa mshahara wa mwezi mmoja kufuatia madai ya utovu wa nidhamu aliouonyesha wa kutofika klabuni kwa wakati.
Niyonzima ambaye alisajiliwa Simba msimu uliopita akitokea Yanga kwa dau la shilingi milioni 113, aliingia mgogoro na uongozi wa klabu hiyo ambapo hakuwa miongoni mwa wachezaji waliokwenda nchini Uturuki katika kambi ya wiki mbili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu.
Hivi karibuni kiungo huyo ilielezwa kuwa aliandika barua ya kuomba msamaha kwa viongozi wa Simba kutokana na kosa la kuchelewa kufika ambapo tayari ameshasamehewa na kilichobakia hivi sasa ni kuitwa katika kamati ya maadili ili kuhojiwa.
Taarifa ambayo Championi Jumatano imezipata kutoka Simba zinasema kuwa, huenda kiungo huyo akapewa adhabu ya kukatwa mshahara wa mwezi mmoja kutokana na kosa alilolifanya kisha ndiyo ajiunge na wenzie kuendelea na ligi.
“Niyonzima ataitwa katika kamati ya maadili ili kuweza kumalizia pale ambapo mazungumzo yalifikia na atapewa adhabu ya kukatwa mshahara wa mwezi mmoja ili aweze kurejea kikosini.
“Uongozi tayari umeshakubaliana na msamaha wake hivyo kila kitu kipo vizuri na wakati wowote kuanzia sasa atajiunga na timu,” kilisema chanzo hicho.
Aidha Niyonzima kwa sasa yupo nchini kwao katika majukumu ya timu ya taifa ambapo akirejea tu suala hilo linatafutiwa ufumbuzi.