Kuelekea pambano la watani wa jadi Simba na Yanga litakalopigwa Jumapili, Septemba 30, 2018, timu hizo zimebadilishana maeneo ya kambi baada ya Simba kubaki jijini Dar es salaam huku Yanga wakienda mkoani Morogoro.
Kabla ya mchezo wa marudiano wa msimu uliopita timu hizo zilikuwa zimeweka kambi katika maeneo tofauti yakifanana na msimu huu. Yanga waliweka kambi Dar es salaam huku Simba wakienda Morogoro. Baada ya kukutana mchezo huo ulimalizika kwa Simba kushinda bao 1-0 likifungwa na Erasto Nyoni dakika ya 37.
Yanga SC imeondoka jana kwenda Morogoro kwa ajili ya kambi ya kujiandaa na mchezo huo ikiwa ni siku moja tangu ishinde mabao 2-0 dhidi ya Singida United. Wakati huo Simba wametua jana jioni jijini Dar es salaam wakitokea mkoani Shinyanga ambako walishinda mabao 3-1 dhidi ya Mwadui FC Jumapili.
Kwenye mechi ya kwanza ya msimu uliopita iliyopigwa Oktoba 28, 2017, timu hizo zilitoka sare ya 1-1. Simba walitangulia kwa bao la Shiza Kichuya dakika ya 57, kabla ya Obrey Chirwa kuisawazishia Yanga dakika ya 60.
Mpaka sasa Simba SC imecheza mechi tano, ikishinda tatu sare 1 na kufungwa 1 wakati wapinzani wao Yanga wamecheza mechi 4 na kushinda zote