Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amepingana na baadhi ya mashabiki wanaouita mchezo wa Simba na Yanga 'Kariakoo derby' kuwa wanakosea kwasababu Simba pekee ndio inatokea Kariakoo na sio Yanga.
Kupitia maelezo yake, Manara amefafanua kuwa kuita mchezo huo kariakoo Derby ni makosa kwani Yanga ni klabu iliyopo kata ya Jangwani wakati Simba ipo kata ya Kariakoo hivyo hakuna uhusiano wa Yanga na Kariakoo.
''Yanga haitoki Kariakoo inatoka kata ya Jangwani na Diwani wao ni Mh. Abdallah Faraj huku Simba ikitokea Kariakoo na diwani wetu akiwa Mh. Abulkarim Masamaki'', ameandika Manara.
Manara ameshauri mchezo huo uendelee kuitwa Dar es salaam Derby kwani timu hizo zinatokea Dar es salaam.
Kwenye mchezo wa kesho Jumapili Septemba 30, 2018 Simba watakuwa wenyeji wa Yanga. Mchezo huo ni wa 6 kwa Simba kwenye ligi kuu msimu huu. Yanga wao ni mchezo wa 5 msimu huu.
Simba wameshinda mechi 3, sare 1, na kufungwa 1 wakiwa na alama 10 katika nafasi ya 5. Yanga wameshinda mechi zote 4 na wana alama 12 wakiwa katika nafasi ya 4.