WAKATI sakata la Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma kutaka kufukuzwa ndani ya kikosi cha timu hiyo likiwa bado halijapoa sana, taarifa mpya ni kwamba kocha huyo amepewa masharti magumu ambayo anatakiwa kuyafuata ili kulinda kibarua chake hicho.
Masharti ambayo Djuma raia wa Burundi amepewa ni ya kuhakikisha anafuata utaratibu wa klabu hiyo pamoja na kushirikiana vema na makocha wenzake na kusahau tofauti zao zilizopo.
Chanzo kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Championi Jumamosi kuwa, mwekezaji na mwanachama wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’, ndiye amezuia zoezi hilo la kutimuliwa kwa Djuma huku akitoa masharti hayo.
Chanzo hicho kilienda mbali zaidi na kueleza kuwa, awali Mo Dewji pamoja na viongozi wa juu wa Simba ndio waliokuwa kwenye mpango wa kumtimua kocha huyo, lakini baada ya taarifa hizo kuvuja, wakabadili mawazo.
“Mo ameamua kumuacha Djuma aendelee na badala yake amepewa masharti magumu ya namna ya kuishi karibu na makocha wenzake na lile suala la sare za timu ametakiwa kuhakikisha anazivaa muda wote hadi mkataba wake utakapoisha.
“Mo ameona asimtimue kwa sasa baada ya siri hiyo kuvuja kwani walitaka wafanye kimyakimya, lakini kutokana na siri kuvuja huku pia akimkosa mtu aliyetoa siri hizo, wameamua kubadili mawazo,” kilisema chanzo chetu.