Kikosi cha Simba jana Jumanne kimeweka rekodi mpya ya fedha jijini Dar es Salaam ya kutumia Shilingi milioni tatu kwa ajili ya kupumzika mchana.
Simba ambao wanafanya mazoezi Gymkhana jijini Dar es Salaam imepanga vyumba 20 kwenye hoteli moja ya jijini hapa kwa ajili ya wachezaji wao kupumzika mchana na jioni wakishamaliza mazoezi wanakwenda kulala kwao.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Jumatano lilizipata zimedai kuwa baada ya mazoezi ya jana asubuhi ya timu hiyo katika Uwanja wa Gymkhana, wachezaji pamoja na viongozi wao wa benchi la ufundi walienda katika hoteli hiyo kwa ajili ya kupumzika ikiwa ni pamoja na kupata chakula cha mchana kabla ya kurudi tena uwanjani kuendelea na mazoezi.
“Mazoezi yetu ya asubuhi yalianza saa 2.30 mpaka saa 5.30 asubuhi kisha tukaenda hoteli kwa ajili ya kupumzika kwa masaa mawili baadaye saa 8.00, mchana tukarudi uwanjani kuendelea na mazoezi, baada ya hapo kila mtu akaenda kwake.
“Gharama ambazo zimetumika kwa muda huo ni takriban Shilingi milioni 3,000,000 kwa ajili ya kulipia vyumba pamoja na chakula cha mchana, chai na gharama nyingine ndogondogo.
“Katika programu hiyo, mwalimu pia anasema kulala mchana kwa wachezaji ni sehemu ya programu yake ndiyo maana baada ya mazoezi ya asubuhi wachezaji wanalala, kisha baadaye mazoezi yanaendelea,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusiana na hilo, Meneja wa Simba, Richard Robert, hakuwa tayari kusema chochote ingawa Championi Jumatano linajua ni programu ya Kocha Patrick Aussems ambaye anapambana na muda na foleni za Dar es Salaam ambazo zinaweza kuchelewesha mambo