Simba Yawafuta Machozi Mashabiki...Bocco Afanya Jambo na Kuweka Rekodi
0
September 23, 2018
Baada ya misukosuko ya mechi mbili mfululizo za ligi kuu Tanzania bara, hatimaye Simba imeanza kuwajibu mashabiki wake kwa ushindi wa leo dhidi ya Mwadui Fc mjini Shinyanga.
Mchezo huo umemalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, mabao ya Simba yakifungwa na John Bocco katika dakika ya 41 kwa penalti, dakika ya 45 na dakika ya 50 kupitia kwa Meddie Kagere huku bao pekee la kufutia machozi la Mwadui Fc likifungwa na Charles katika dakika ya 81 ya mchezo.
Mchezo huo umeshuhudia pia mshambuliaji wa Simba, John Raphael Bocco akiweka historia ya kuwa mtanzanian na mchezaji wa kwanza kufunga idadi ya mabao 100 katika historia ya ligi kuu soka Tanzania bara. Alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 80 ya mchezo kwa kumpiga kiwiko beki wa Mwadui Fc.
Baada ya ushindi huo, sasa Simba inafikisha alama 10 na kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu Tanzania bara huku nafasi ya kwanza ikishikiliwa na Azam Fc baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Alliance Fc, bao lililofungwa na Tafadzwa Kutinyu katika dakika ya 59 ya mchezo.
Mchezo wa mapema, umeshuhudia Mbeya City ikitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Mtbwa Sugar katika dimba la Sokoine jijini Mbeya, bao la Mbeya City likifungwa na Eliud Ambokile katika dakika ya 34 huku bao la Mtibwa Sugar likifungwa na Selemani Mangoma katika dakika ya 52 ya mchezo.
Ratiba ya mchezo wa mwisho hii leo itakamilishwa na Yanga itakayochuana na Singida United katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam. Endapo Yanga itafanikiwa kuibuka na ushindi katika mchezo huo itaongoza ligi kwa alama 12, ikiipiku Azam Fc yenye alama 11 kwa alama moja.
Tags