Spika wa Bunge, Job Ndugai amekerwa na wabunge wa CCM na Mawaziri kutotumia mitandao ya kijamii kupeleka majibu na ufafanuzi wa Serikali kwa wananchi kama wafanyavyo wapinzani.
Ndugai alieleza hisia zake jana Septemba 10, 2018 akisema wabunge wa upinzani wamekuwa wajanja katika kutumia mitandao ya kijamii ambayo inasomwa dunia nzima na hivyo kuwaaminisha watu.
Alitoa kauli hiyo wakati Bunge likipitisha muswada wa sheria wa marekebisho ya sheria mbalimbali namba 3 wa 2018.
"Kuna katabia kamezuka humu, wabunge wanaishambulia Serikali lakini inapokuja muda wa kujibu wanakuwa hawapo, lakini wanakuwa wameshashinda maana wanakuwa wametuma kwenye YouTube na watu dunia nzima wanasoma lakini ninyi (wabunge wa CCM) hakuna, utakuta hata ufafanuzi wa mawaziri hakuna," alisema Ndugai.
Alisema ni wakati sasa wabunge wa CCM na mawaziri kujipanga na kutumia mitandao ipasavyo ili dunia ijue mambo mazuri ya Bunge la Tanzania na hapo ndipo watu watapata ufafanuzi kwa maswali ya upande wa pili.