WAZIRI Mkuu Mstaafu na Mwenyekiti wa Chadema kanda ya Pwani, Fredrick Sumaye amerusha kombora kwa chama chake cha zamani CCM, akisema kama kitaendelea kuongoza nchi basi wananchi watarajie kuingia kwenye kipindi kigumu zaidi cha maisha.
Sumaye ambaye alihamia Chadema mwaka 2015 katika vuguvugu la mabadiliko kwenye uchaguzi mkuu uliopita amesema licha ya wananchi walio wengi kulalamika kuwa maisha yamekua magumu bado wanapaswa kutambua kuwa yatazidi hivi sasa endapo wataendelea kuipigia kura CCM.
Hayo ameyazungumza leo wakati akimnadi mgombea Ubunge jimbo la Ukonga, Asia Msangi ambapo alisema yeye mwenyewe aliamua kuondoka CCM baada ya kuona kuwa chama hicho hakina dhamira ya kweli ya kuwaletea maendeleo wananchi.
" Wananchi mnalalamika vyuma vimekaza, lakini mimi nawaambia hali ya sasa hivi ni nzuri kuliko huko tunakokwenda, kama hamtoamua kuitoa CCM madarakani basi jiandae kuumia zaidi ya sasa, vyuma sasa bado havijakaza vimepinda," amesema Sumaye.