Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea kupokea salamu za rambirambi kutoka kwa marais, mawaziri wakuu wa mataifa mbalimbali duniani kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere iliyotokea kwenye Ziwa Victoria, Mkoani Mwanza tarehe 20 Septemba, 2018 na kusababisha vifo, majeruhi na upotevu wa mali.
Baadhi ya salamu zilizopokelewa ni pamoja na kutoka kwa Rais wa Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, Rais wa Urusi, Mheshimiwa Vladmir Putin, Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Ujerumani, Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier, Rais wa Saharawi, Mheshimiwa Brahim Ghali, Mtawala wa Kuwait, Mtukufu Sheikh Sabah Al-Ahmad al Jaber Al-Sabah, Baba Mtakatifu, Papa Francis, Rais wa Italia, Mheshimiwa Sergio Mattarella, Rais wa Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan, Rais wa Finland, Mheshimiwa Sauli Niinistö, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mheshimiwa Joseph Kabila Kabange na Rais wa Jamhuri ya Sudan, Mheshimiwa Omar Hassan Ahmed Al-Bashir.
Viongozi wengine ni Waziri Mkuu wa Israel, Mheshimiwa Benjamin Netanyahu, na Waziri Mkuu wa Sweden, Mheshimiwa Stefan Löfven.
Viongozi hao wameeleza kusikitishwa kwao na taarifa za vifo vilivyosababishwa na ajali hiyo na kuwatakia majeruhi kupona haraka.
Sehemu ya nukuu za salamu hizo zinasema “Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, nilipokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyosababisha vifo vya watu wengi, majeruhi na wengine kutojulikana walipo. Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Kenya naomba upokee na kufikisha salamu zetu za rambirambi kwa wafiwa na wananchi wote wa Tanzania kufuatia ajali hiyo na tunawaombea majeruhi wote wapone haraka” ni sehemu ya nukuu ya salamu kutoka kwa Mheshimiwa Rais Kenyatta
“Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, nilishtushwa na taarifa za ajali hiyo mbaya iliyotokea Mkoani Mwanza. Kwa niaba ya Serikali ya China, wananchi na mimi binafsi natoa pole kwa wafiwa wote na majeruhi” inasema sehemu ya salamu kutoka kwa Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping.
Naye Rais wa Urusi, Mheshimiwa Putin amesema “Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, tafadhali naomba upokee salamu zangu za rambirambi kufuatia ajali iliyotokea. Naomba salamu hizi ziwafikie wafiwa wote na ninawaombea majeruhi wapone haraka”
Aidha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea salamu za rambirambi kutoka kwa balozi mbalimbali zinazowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini, ikiwemo ubalozi wa Marekani, ubalozi wa Ufaransa, ubalozi wa Sudan Kusini, Ubalozi wa Falme za Kiarabu (UAE), Serikali ya Brazil, Ubalozi wa Cuba, ubalozi wa Nigeria na salamu kutoka kwa Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Kimataifa nchini.
Wakati huohuo, Wizara imepokea salamu za rambirambi kutoka kwa mabalozi wanaowakilisha Tanzania kwenye nchi mbalimbali. Salamu zilizopokelewa zinatoka kwa mabalozi wote wa Tanzania katika nchi za Qatar, Ufaransa, Uingereza, Uholanzi, Afrika Kusini, Sweden, Nigeria, Burundi, Uganda, Kenya, Ubelgiji, Zambia, Msumbiji, China, Japan, Brazil, Comoro, Algeria, Sudan, Canada,
Kadhalika tumepokea salamu kutoka kwenye balozi zetu zilizoko Marekani, Uturuki, Rwanda, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, Kuwait, Saudi Arabia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zimbabwe, Malawi, Uswisi, India, Italia, Jamhuri ya Korea, Urusi, Israel, Ethiopia, Ujerumani, Oman na Malaysia.
Baadhi ya nukuu ya salamu za rambirambi za mabalozi hao zinasomeka kama ifuatavyo “Inna Lillah Wainna Illah Rajiuon. Kwa niaba ya Ubalozi Abuja na Watanzania waliopo katika eneo letu la uwakilishi, tunatoa pole kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, familia na Watanzania kwa ujumla kwa msiba mkubwa uliotufika. Mwenyezi Mungu atupe subira na faraja katika kipindi hiki cha majonzi na aziweke roho za marehemu mahali pema na majeruhi wapone haraka, Amin Amin,” ni kauli yake Mheshimiwa Muhidin Ally Mboweto, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mheshimiwa Dkt. Wilbroad Slaa anasema “kwa niaba ya wenzangu katika kituo cha Stockholm tunatoa pole za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndugu na familia zote zilizoguswa na msiba huu mkubwa. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi na kuwatia nguvu na ujasiri ndugu wote walioguswa na msiba huu”.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Balozi Modest Mero alisema haya; “Ubalozi wa New York tunatoa pole kwa ajali mbaya ya Meli ya MV Nyerere iliyopelekea wengi kupoteza maisha na wengi kuumia. Tunawaombea marehemu pumziko la milele na wote waliojeruhiwa wapone haraka.”
Balozi wa Tanzania nchini China, Mheshimiwa Mbelwa Kairuki alieleza masikitiko yake kwa kusema kuwa “nasi huku Beijing tunaungana na wenzetu kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Watanzania na wanafamilia walioguswa msiba huu mzito. Mwenyezi Mungu awape nguvu na awajalie moyo wa subira wakati wote mnaposhughulika na msiba huo.
“Japan na diaspora yetu tunatoa pole kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wote kwa msiba huu uliotokana na kuzama kwa kivuko. Mungu atupe nguvu wote tuliobaki na awape pumziko la amani wenzetu waliotutangulia. Kwa majeruhi tunawaombea wapone haraka na wavumilie mstuko huu mkubwa katika maisha yao. Marehemu wapumzike kwa amani”. Hizi ni salamu kutoka kwa Mheshimiwa Mathias Chikawe, balozi wa Tanzania nchini Japan.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Abu Dhabi alisema haya; “Ubalozi wa Tanzania Abu Dhabi, tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali ya MV Nyerere.Kwa niaba ya watumishi wote wa Ubalozi, tunatoa mkono wa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania wenzetu wote kwa msiba huu mkubwa. Mwenyezi Mungu awajaalie marehemu wapumzike mahali pema na awajaalie majeruhi kupona mapema. Amin”.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mheshimiwa Dkt. Asha-Rose Migiro akieleza kuguswa na ajali hiyo alitoa kauli hii “Ubalozi wa Tanzania London unajumuika na Watanzania wenzetu kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, familia na ndugu wa wale wote waliopatwa na msiba kutokana na ajali hii. Tunawaombea majeruhi wapone haraka na warejee katika shughuli zao za kujikimu na kulijenga taifa letu”.
Kwa upande mwingine, Wizara imepokea salamu za rambirambi kutoka Baraza la Diaspora wa Tanzania ulimwenguni kote (TDC Global) ambao wameeleza masikitiko makubwa kufuatia ajali hiyo mbaya. Sehemu ya ujumbe wao unasomeka kama ifuatavyo; “TDC Global, kwa masikitiko makubwa, inatoa salamu za rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania wote, ndugu, jamaa na marafiki kwa vifo vilivyotokana na ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV. Nyerere kinachofanya safari zake kati ya visiwa vya Bugorora na Ukara katika Ziwa Victoria. Kama TDC Global, tunaungana na Watanzania wote katika kuomboleza msiba huu mzito kwa taifa letu. Pia tunatoa pole kwa majeruhi wote na kuwaombea wapone haraka”.