Tatizo la Afrika sio China. Sio Ulaya. Sio Marekani: Tatizo la Afrika ni Waafrika wenyewe


Na Zitto Kabwe, Mb

Ushirikiano kati ya nchi za Kiafrika na Taifa linalokua kwa kasi la China umekuwa ni mjadala mkubwa duniani. Vyombo vya habari, hasa vya nchi za magharibi, vimekuwa na vinaandika makala mbalimbali kuhusu hatari ya Afrika kutawaliwa na China. Wanaita ni ukoloni mamboleo. Makala hizi zimedakwa na vyombo vya habari vya Afrika na hata wanasiasa na watunga sera na kujikuta wanarudia kama kasuku ubaya wa China kwa Afrika. Ni muhimu niseme mapema kuwa, mahusiano ya nchi za Afrika na China yana changamoto kama ilivyo kwa mahusiano ya Afrika na nchi nyengine yeyote kubwa. Vile vile mahusiano hayo yaweza kuwa na faida kama ilivyo kwa mahusiano ya Afrika na nchi nyengine yeyote kubwa. Hivyo inatupasa kuwa makini kwenye mjadala huu ili kuepuka kumezeshwa ubaya au uzuri wa China kutoka kwa wengine.

Mwalimu Julius Nyerere, Rais kwa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitembelea China mwezi Februari mwaka 1965. Akiwa Peking (sasa Beijing), Mwalimu alihutubia mkutano wa hadhara. Katika mkutano huu alisema “tunaambiwa kuwa Wachina ni watu hatari sana, kuwa wana akili sana kiasi kwamba mafundi wao wachache wanaweza kuidhuru nchi yetu yote, kwa hiyo tusiwe karibu nao kabisa. Tuliwaambia ( hao wanaotuambia ), na ninawaambia tena sasa- huo ni upuuzi”. Upuuzi aliousema Mwalimu Nyerere mwaka 1965 bado unaendelea katika karne ya 21. Hata hivyo hakuna upuuzi ulio upuuzi mtupu, hata katika upuuzi kuna jambo la kujifunza. Katika makala haya tunatazama machache kuhusu ‘upuuzi’ huu na kutahadharisha kuwa tatizo letu sio China au Taifa lengine lolote bali ni Afrika yenyewe.

Hofu mkubwa wa wachambuzi wa masuala ya Sino-Afrika na hata raia wa nchi mbalimbali za Afrika ni mikopo yenye lengo la kutwaa mali ikiwemo maliasili kama madini na hata Mashirika ya Umma. Wanaita ‘debt trap diplomacy’. Hii ni hofu inayoeleweka hasa baada ya kushuhudia nchi ya Sri Lanka ikipoteza Bandari yake moja kwa kushindwa kulipa deni la China. Hata hivyo, kama alivyosema mwanazuoni Deborah Brautigam kwenye kitabu chake cha The Dragons Gift: The real story of China in Africa, habari hizi zimejaa chumvi kwenye ukweli na hata kwenye uzushi. Moja ya uzushi ni kuhusu habari za baadhi ya Mashirika ya Umma Zambia kuwa yamechukuliwa na China. Hii hofu ya mikopo ina ukweli kiasi gani?

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kimarekani ya Center for Global Development ( CGD) na kuandikwa na W. Gyude Moore unaonyesha kuwa China sio nchi kiongozi kwenye mikopo kwa Afrika na kusababisha matatizo makubwa ya madeni kwa nchi za Afrika. Lakini vyombo vya habari vya dunia vinasambaza kwa kasi hii dhana ya ‘debt trap diplomacy’. Moore anasema “ hii lugha ya mtego wa diplomasia ya madeni inazungumzwa zaidi kwenye nchi za magharibi na Marekani kwa sababu msingi wake ni ‘wasiwasi kuhusu China kuwa Taifa lenye nguvu duniani..”. Ametoa takwimu kuwa deni la Afrika kwa China ni USD 115 Bilioni kati ya mwaka 2000-2016 ambayo ni 2% tu ya Deni la Afrika kwa nchi nyengine za dunia nzima. Kwanini deni dogo namna hii lipigiwe kelele nyingi?

Hapa Tanzania takwimu za Deni la Taifa hazipo wazi sana na hivyo kuwa na ugumu wa kufanya uchambuzi wa kina. Kuna haja ya Serikali kutoa Taarifa rasmi ya kiwango cha deni letu kwa China. Hata hivyo Taarifa ya Benki Kuu ya robo Mwaka unaoishia Juni 2018 inaonyesha kuwa Mashirika ya Kimataifa yanachangia 46.5% ya Deni la nje la USD 20.5 bilioni ( Shilingi 45.7 trilioni ). Mikopo ya Nchi ‘bilateral’ ikiwemo China ni 9% ya Deni zima na Mikopo ya kibiashara ni 32% ya Deni zima la nje. Ndani ya Mikopo ya kibiashara kuna mikopo kutoka Benki za China kwa hakika ( Mfano mkopo wa Exim Bank kwenye Bomba la Gesi kutoka Mtwara kuja Dar, Mkopo wa Nyumba za Jeshi nchi nzima na mkopo wa Mkonga wa Taifa ). Kwenye mikopo hii ya Biashara kuna mikopo pia ya Benki za nchi za Magharibi kama vile Credit Suisse, Standard Bank na nyengine ambayo ni sehemu kubwa ya Deni letu la Nje tangu mwaka 2016 maana ndani ya muda huo hatujakopa kutoka China. Serikali ikiweka wazi orodha ya wanaotukopesha tutaona kuwa sehemu ya Deni la Taifa kutoka China yaweza kuwa chini ya 10% ya Deni lote la nje. Hivyo wasiwasi wa Tanzania haupaswi kuwa China, bali ni Mashirika ya Kimataifa kama Benki ya Dunia na Benki za Magharibi ambazo zinakimbilia kutupa mikopo ghali. Juzi tu Benki ya Standard Chartered imetangaza kutupa mkopo wa USD 1.5 Bilioni ( Shilingi 3.3 trilioni ) kwa ajili ya ujenzi wa Reli. Mikopo ya Kibiashara ni hatari zaidi kuliko mikopo nafuu kutoka kwenye nchi rafiki. 

Hofu nyengine ni ajira. Kumekuwa na hofu kubwa miongoni mwa Waafrika kuwa Wachina wanaopata mikataba ya ujenzi wa miundombinu huleta mpaka wafungwa kuja kufanya kazi na kutosaidia Waafrika kupata ajira. Mwandishi Howard French ameandika kuhusu hili la mamilioni ya Wachina wanavyoligeuza bara la Afrika kuwa nyumbani kwao. Katika Kitabu hiki China’s Second Continent, French anamnukuu msomi Ed Brown kutoka Ghana kuwa “ mahusiano haya [ na China ] yanakwenda kuamua kuhusu hatma ya Afrika katika miaka hamsini ijayo. Swali la msingi ni kama Afrika imejiweka tayari kufaidika na mahusiano haya au tutaishia kuwa ‘koloni’ la watu wengine tena”. Serikali za nchi za Afrika ndio zinazotunga sheria za kazi na mahusiano kazini na sio Serikali ya China wala hatulazimishwi na China. Hofu ya Ajira na kujaa kwa Wachina hapa Afrika inadhibitika kwa kuhakikisha kuwa Serikali za Afrika na Waafrika wanasimamia sheria zao wenyewe.

Hii hofu ya Wachina kujaa Afrika sio hofu mpya. Wakati wa ujenzi wa TAZARA miaka ya 1970 kulikuwa na hofu hii pia. Katika Kitabu cha A Monument to China-Africa Friendship: Firsthand Account of the Building of the TAZARA, Rais Benjamin Mkapa anaeleza namna alivyotumika kuondoa hofu hii kwa Watanzania wakati yeye ni Mhariri wa magazeti ya Serikali. Anasema, “kulikuwa na hisia kubwa miongoni mwa watu wetu kuwa Wachina watajaa nchini na kutuzidi idadi na kuichukua nchi yetu. Watu walikuwa na wasiwasi kwelikweli kwani hatukuwa na Wachina wengi nchini kwetu na wengi hawakuwa wamewahi kuwaona Wachina. Tuliwaambia, msiwe na wasiwasi. Kujenga Reli huhitaji Wachina wote kuja hapa”. Ikumbukwe kuwa Mradi huu wa TAZARA ulipingwa na Benki ya Dunia na nchi za magharibi na hivyo magazeti yao, kama ilivyo sasa, yalijaza hofu kwa Watanzania kuwa Wachina wanawavamia. Hii ni miaka ya 1970 na ushahidi sasa upo wazi kuwa Wachina hawajatuzidi kwa idadi. Ilikuwa hofu tu. 


Ninaamini kuwa Waafrika tunapaswa kutafakari wenyewe namna tunajenga mahusiano na China. Tukwepe kuelekezwa na mataifa mengine lipi bora kwetu au baya kwetu kama ambavyo tunapaswa kukwepa kuingia kwenye miradi ambayo haina maana yeyote na haswa iliyogubikwa na rushwa. Kwa mara ya pili China imetangaza uwekezaji wa USD 60 bilioni ( shilingi 133 trilioni ) katika Mkutano wa FOCAC huko Beijing mwezi huu wa Septemba 2018. Mwaka 2015 katika mkutano kama huo wa FOCAC China ilitangaza pia kiasi kama hicho cha Fedha kwa ajili ya Maendeleo ya Afrika. Fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya mikopo nafuu (USD 35bn), Misaada ( USD 5bn), Mikopo ya USD 5bn kwa Kampuni ndogo na za kati ( SMEs) na USD 15bn kama Mtaji kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo wa China-Afrika. Tayari nchi kama Afrika Kusini imeshaingia Mkataba wa USD 20bn kutoka fedha hizi kwa ajili ya kutatua matatizo yake ya Uchumi. Sisi Tanzania kabla ya kuanza kutaka kufaidika na ahadi hizi mpya tunapaswa kuelezwa kama tulifaidika na ahadi za mwaka 2015. Kwa utafiti wangu niliyoufanya hatukufaidika moja kwa moja. 

Mpango ulikuwa ni kuchukua mkopo nafuu kujenga Reli ya Kati ya kisasa lakini bahati mbaya Serikali iliamua kutochukua mkopo huo nafuu na badala yake kutumia fedha za kodi ( na kuleta madhara makubwa ya mzunguko wa fedha nchini ) na kuchukua mikopo ya kibiashara kutoka kwenye Benki za magharibi kama Credit Suisse na Standard Chartered. Taarifa nyengine ni kuwa sehemu ya gharama za ujenzi wa Reli kutoka Dar kwenda Morogoro Mkandarasi, Kampuni ya Kituruki, amekwenda kukopa China kwa riba kubwa zaidi ya riba ambayo Tanzania ingepewa na hivyo kujikuta sisi wenyewe tunalipa mkopo huo kupitia kulipia gharama za ujenzi kwa Mkandarasi huyo. Serikali yetu itachukua fursa hii ya sasa kutoka China kuanza ujenzi wa Reli Dodoma-Tabora-Mwanza? Hakuna anayefahamu kwani inaonyesha sera yetu ya sasa ni kupunguza kukopa kutoka China ambapo hakika tumekopa chini ya 10% ya Deni la Nje. Mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kuongeza Mikopo ya Kibiashara kutoka kwenye Mabenki ya nchi za Magharibi, angalau uzoefu unaonyesha hivyo.

China ilikuwa nchi masikini sana wakati inatusaidia kujenga TAZARA ili kukwepa mbinu za utawala wa makaburu dhidi ya ukombozi wa kusini mwa Afrika. Zhou Nan, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China wa wakati huo anaeleza kwanini waliamua kuisaidia Tanzania na Zambia licha ya hali yao mbaya kiuchumi kufuatia majanga ya kiasili, uchumi dhaifu na hali ngumu ya maisha ya watu wake. Nan anasema “ China ilikuwa na hali ngumu sana na kulikuwa na vitu vingi vya kufanya kwa ajili yetu wenyewe. Hata hivyo, Serikali ilikuwa na mwono wa kimkakati ( strategic view ) na kuamua kuwa ni lazima kusaidia marafiki zetu wa Afrika. Ni lazima tusaidie hata kama tutakula na kutumia kidogo zaidi sisi wenyewe […..]. Tanzania ni rafiki yetu, wakiwa na nguvu, na sisi tutakuwa na nguvu”. Mwenyekiti Mao alimwambia Mwalimu Nyerere “ Ninyi mna matatizo, kama sisi tu. Lakini matatizo yenu ni tofauti na ya kwetu. Tutawasaidia kujenga hii reli hata kama hiyo maana yake ni sisi kuchelewa kujenga reli nchini kwetu”. TAZARA ikajengwa namna hii. 

Inaumiza sana kuwa sisi wenyewe Waafrika tumeshindwa kuiendesha TAZARA licha umuhimu wake mkubwa wa kihistoria katika ukombozi Kusini mwa Afrika. Tunapaswa kujifunza kwa miradi mipya ili kuepuka upotevu mkubwa unaoweza kutokea. Kwa mfano tulikopa USD 1.3bn kutoka China ili kujenga Bomba la Gesi la Mtwara – Dar es Salaam. Tunatumia Bomba hili 6% tu kwa mujibu wa CAG na tunaanza mradi mpya wa Stiglers Gorge kwa shabaha ile ile ya kuzalisha Umeme. Matumizi ya 30% tu ya Bomba hilo yanaweza kutupati mara mbili ya Umeme wote kutoka Rufiji kwa kiwango kile kile cha fedha tunazowekeza huko Rufiji. Imebakia miaka 2 kuanza kulipa mkopo huu wa Bomba ilhali matumizi yake ya 6% hayawezi kuzalisha mapato ya kutosha kuhudumia deni hilo. Haya ndio matatizo ya Waafrika. Hili sio tatizo la mkopo kutoka China. Ni tatizo letu!

Nasaha zangu kuhusu mahusiano yetu na China ni kujitazama sisi wenyewe tunataka nini na tunapataje tunachotaka badala ya kuimba kama kasuku tunayoambiwa kuhusu mahusiano yetu na China. Miaka na miaka tumekuwa na mahusiano na Nchi za Magharibi ( kwanza kwa kututawala kama makoloni yao, kutupa mikopo ili kuwa upande wao kwenye vita baridi ( kumbuka Zaire ya Mobutu na Marekani nk ) na hali yetu duni ipo pale pale. Tatizo la Afrika sio nani tunahusiana naye, Tatizo la Afrika ni Waafrika wenyewe. Tusikilize ukosoaji wa wengine dhidi ya China lakini tuamue wenyewe kwa maslahi ya maendeleo ya watu wetu. 


Katika hotuba ya Mwalimu Nyerere niliyonukuu mwanzoni mwaka makala haya, aliendelea kusema maneno ambayo yanapaswa kuwa msingi wa sera yetu ya mambo ya nje kuhusu China, alisema “ Tutaona wenyewe kusudio la China kwetu. Hatutaki kuambiwa na wengine “. Waafrika wanapaswa kutambua wenyewe changamoto za mahusiano kati ya China na Afrika na waamue namna ya kuyatatua badala ya kuimbishwa na mataifa mengine na kuelekezwa kama watoto wadogo ambao hawajitambui licha ya kuwa huru miaka 50 na zaidi. Afrika inajitambua, ina raia wasomi wakubwa wenye uwezo wa kupambanua mambo. Kuendelea kuihubiria Afrika juu ya mahusiano yake na China ni matusi na mwendelezo wa ‘colonial mentality’ kuwa Ulaya na Marekani ndio zinajua zaidi na zinaendelea ‘kutulea’. Jambo muhimu ni Viongozi wa Afrika kutambua wajibu wao, kujifunza kutokana na historia ya mahusiano yetu na nchi za magharibi na kuepuka makosa ya viongozi wa nyuma. Pia Raia wa Afrika kuwajibisha Viongozi wao kwa kuendelea na harakati za demokrasia na haki.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad