Tume ya vyuo vikuu nchini (TCU), imewatoa hofu na mashaka wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini kwa kuwaongezea muda wa siku moja, kwa lengo la kutatua changamoto walizokumbana nazo kwenye zoezi la kuthibitisha pamoja masuala mengine.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka wa TCU Dkt. Kokuberwa Mollel alipokuwa anazungumza East Africa BreakFast, inayorushwa na East Africa Radio leo Septemba 06, 2018, baada ya kuwepo malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wakiulalamikia mfumo wa mtandao wa kuthibitisha chuo kutofanya kazi ipasavyo.
"Ningependa kuwatoa hofu waombaji ambao wamechaguliwa chuo zaidi ya kimoja, kwamba tumeongeza muda hadi leo saa 6:00 usiku kwa lengo la kuwaruhusu wale waliokuwa na changamoto ndogo ndogo ziweze kutatuliwa pamoja na kuweza kujithibitisha", amesema Dkt. Mollel.
Pamoja na hayo, Dkt. Mollel ameendele kwa kusema "kwa wale ambao wameshindwa kujithibitisha tunawashauri kwamba wawasiliana moja kwa moja na vyuo ili kama tatizo litakuwepo ndani ya chuo husika wapate kulitatua, na kama endapo litakuwa nje ya chuo basi chuo husika kitawasiliana na tume ya vyuo vikuu ili tuweze kutatua changamoto kwa pamoja".
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na changamoto nyingi wanazozipata wanafunzi wanaoomba nafasi za masomo kupitia mtandao wa TCU, kutokana na kutojua mfumo huo unahitaji kitu gani huku wengine wakisahau kujaza baadhi ya vitu muhimu na kujikuta wanakosa nafasi za kusoma katika mwaka walioomba na kujikuta wakitoa lawama kwa mamlaka zinazohusika na suala hilo.