Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF linapanga kuleta mkakati pamoja na hamasa mpya kuanzia katika mchezo wa kufuzu michuano ya AFCON dhidi ya Cape Verde utakaopigwa mwezi ujao.
Cape Verde itakuwa mwenyeji dhidi ya Taifa Stars, 12 Oktoba mjini, Praia nchini humo kabla ya timu hizo kurudiana, 16 Oktoba jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia mchezo huo pamoja na maandalizi ya kambi ya Taifa Stars, afisa habari wa TFF, Cliford Mario Ndimbo amesema kuwa watashauriana na mdhamini mkuu wa Taifa Stars ili kuona namna ya timu hiyo ikirejea nyumbani haraka mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo ili kujiandaa na mchezo wa marudiano utakaopigwa jijini Dar es Salaam.
Pia katika mazungumzo hayo watazingatia suala la mashabiki wataopenda kwenda kuisapoti timu yao kuona namna gani watakavyofika nchini Cape Verde lakini pia kiasi kidogo cha nyongeza watakachochangia ambacho kitawafanya kuweza kumudu.
Pia, Ndimbo amezungumzia kuhusu kambi ya Taifa Stars na kikosi kwamba suala hilo litakuja kuzungumziwa na walimu na itazingatia muda wa mchezo huo wa kwanza pamoja na msuala mengine yanayohusiana na mchezo huo.
Amewataka watanzania kuisapoti zaidi timu yao ya taifa kwa kushirikiana na TFF na wadau wote wa soka huku akisisitiza kuwa kuelekea katika michuano hiyo nchini Cameroon, TFF imendaa ‘Hashtag’ maalum itakayoitwa #AFCONCameroon2019Zamuyetu, ambayo itatumika kama kampeni kuhakikisha Taifa Stars inafuzu na kuliwakilisha taifa katika michunao hiyo.