Wakati Yanga wakiwa katika sintofahamu ya kufanya uchaguzi mkuu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema lipo njia panda juu ya kinachoendelea ndani ya klabu hiyo mpaka sasa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikishi hilo, Wakili Revocatus Kuuli, amesema wao kama TFF bado wapo njia panda kwa maana walisema watamrejesha Yusuf Manji kuwa Mwenyekiti wao.
Kuuli ameeleza wao kama TFF walitoa siku 75 kwa Yanga na Simba kuanza michakato ya kujiandaa na chaguzi zao lakini baadaye Yanga wakasema wao bado wanamtambua Manji kuwa ndiye Mwenyekiti.
Mwenyekiti huyo amefunguka kuwa TFF inashindwa ifanye maamuzi yapi kutokana na suala hilo kuchanganya mambo baada ya Manji ambaye baadaye alitangaza kuachia ngazi hiyo kuja kuelezwa tena anarejeshwa.
Mpaka sasa Manji licha ya kuhudhuria mechi ya kimtaifa ya Kombe la Shirikisho kati ya Yanga dhidi ya USM Alger Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, bado hajatoa tamko la kurejea kwake kwenye nafasi hiyo ya Uenyekiti.