Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari katika baadhi ya maeneo ya nchi kuwepo na vipindi vya mvua kubwa kwa saa 24 zijazo.
Taarifa iliyotolewa Septemba 26 na TMA imeeleza kuwa vipindi vya mvua kubwa vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
“Mawimbi makubwa yanayozidi mita mbili yanatarajiwa katika maeneo ya ukanda wote wa Pwani, huku upepo wa pwani ukitarajiwa kuvuma kwa kasi ya kilomiya 30 kwa saa kutoka Kusini – Mashariki kwa Pwani ya Kaskazini na kutoka Mashariki kwa Pwani ya Kusini,” ilisema taarifa hiyo.
Hali ya bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi makubwa kiasi na matazamio kwa siku ya Ijumaa Septemba 28 ni kuendelea kwa mvua katika maeneo ya ukanda wa Pwani ya Kaskazini.
“Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani inatarajiwa kuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua katika maeneo machache na vipindi vya jua, huku mikoa ya Kagera na Geita ikitarajiwa hali ya mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache na vipindi vya jua,” ilieleza taarifa hiyo.