Ujerumani imekuwa nchi ya kwanza kufungua ofi si ndogo mjini Dodoma, iliyozinduliwa mjini hapa jana.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa ofisi hiyo ya mawasiliano, ambayo itafanya pia shughuli za kibalozi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Augustine Mahiga alisema hatua hiyo ni ishara chanya kwa nchi nyingine kufungua ofisi zao jijini Dodoma.
“Tunajua Umoja wa Mataifa umefungua ofisi yake ya mawasiliano hapa jijini Dodoma, lakini kwa upande diplomasia ninyi (Ujerumani) mmekuwa wa kwanza kufungua ofisi ndogo na huu ni mwelekeo mzuri wa kuhamia kabisa jijini hapa na pia ni ishara chanya kwa mataifa mengine kuhamia Dodoma,” alisema.
Mahiga aliongeza, mara nyingi historia inajirudia, wakati leo (jana) tunasherehekea uzinduzi wa ofisi ndogo ya ubalozi wa Ujerumani, takribani miaka 100 iliyopita Ujerumani walikuwa wakisherehekea kufikia nusu ya ujenzi wa Reli ya Kati.”
Alisema Ujerumani imekuwa na uhusiano wa miaka mingi na kuwa nchi ya kwanza kuiingiza Tanzania kwenye uchumi wa dunia.
Mahiga aliiomba Ujerumani kuwa mstari wa mbele na mbia wa kuisemea Tanzania katika mashirika ya kimataifa kama Umoja ya Ulaya (EU), na Baraza la Umoja wa Mataifa la Ulinzi na Usalama na kuongeza kuwa ajenda zote za nchi, zitakuwa zikijadiliwa hapa nchini.
Balozi wa Ujerumani nchini, Dk Detlef Waechter alisema ofisi yake imefungua ofisi ndogo ya Wakala wa Ujerumani wa Maendeleo (GIZ) na (KFW) pamoja na Ubalozi wa Ujerumani uliopo Dar es Salaam baada ya kuwapo kwa ongezeko la uhitaji.
“Karibu serikai yote ya Tanzania imeshahamia katika mji mkuu, tumeona ongezeko la uhitaji wa kutafuta njia ya kuendeleza ushirikiano katika nyanja zote kwa kiwango kile kile, ukaribu na urafiki wetu,” alisema.
Aliongeza: “Hii ndio sababu watendaji watatu wa Ujerumani katika nchi hii wameungana na kusema tufanye mpango wa kufungua uwakilishi Dodoma”.
Dk Waechter alisema Ujerumani inajua kuwa nchi kuhamisha makao yake makuu huchukua muda mrefu na kupitia changamoto kadhaa. Alitoa mfano hatua ya nchi yake iliyohamisha makao makuu yake kutoka mji wa Bonn kwenda Berlin.
“Tukiwa katika mwaka wa 30 tangu kuanza kuhamisha Makao Makuu ya nchi, asilimia 50 ya watumishi wa serikali bado wanafanya kazi zao si katika mji mkuu mpya wa Berlin, ila bado wako Bonn.”
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge aliwahakikisha ulinzi na usalama kwa Mkoa wa Dodoma na kuongeza kuwa serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuboresha miundombinu na huduma ili kuhakikisha watu wa mataifa yote wanaishi wa usalama.