Sumu anayodaiwa kunyweshwa staa wa Bongo Fleva, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ kwenye kinywaji imeibua hatari iliyopo kwa mastaa wengine Bongo hasa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Ali Salehe Kiba ‘King Kiba’ambao huenda nao yakawakuta yaliyomkuta mwenzao wasipokuwa makini. Dimpoz alipata tatizo kwenye koromeo na kushindwa kumeza chakula ambapo alifanyiwa operesheni nchini Afrika Kusini na sasa yupo mjini Mombasa, Kenya akiendelea kuuguza kidonda kilichopo shingoni.
DIAMOND, KIBA HATARINI KIVIPI?
Kwa mujibu wa Dimpoz, yeye hakumbuki kama ana uadui na mtu yoyote kiasi kwamba amekuwa akiishi kijamaa sana, mazingira ambayo huenda ndiyo yaliyomfanya akawekewa sumu hiyo na wasiomtakia mema. Kwa maelezo hayo, kuna uwezekano pia kilichompata Dimpoz kikawapata pia Kiba na Diamond ambao nao mfumo wao wa maisha hauko tofauti sana na wa Dimpoz.
BABA DIMPOZ AWATAJA KIBA DIAMOND
Akiongea na Risasi hivi karibuni kuhusiana na kilichompata mwanaye, baba wa Dimpoz, Faraji Nyembo alisema: “Alichofanyiwa mwanangu anaweza pia kufanyiwa Diamond au Kiba, wanatakiwa kuwa makini sana maana lazima watakuwa na watu ambao hawawatakii mema kutokana na mafanikio yao hivyo wanaweza pia kuwawekea sumu,” alisema baba huyo.
SIKU 140 ZA MATESO
Kwa mujibu wa Dimpoz, alianza muda mrefu kusumbuliwa na tatizo hilo, lakini Mwezi Mei, mwaka huu ndipo alipoanza siku za mateso na maumivu hadi leo ambapo ni siku takribani 140. Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kwamba mbali na Kiba na Diamond, mastaa wengi wa Kibongo na viongozi mbalimbali wapo kwenye hatari ya kunyweshwa sumu kama aliyonyweshwa Dimpoz kutokana na mazingira wanayopenda kujiachia kwa vinywaji.
ZIPO NYINGI
Uchunguzi huo ulibaini kwamba, zipo sumu za aina nyingi ambazo zinaweza kutumiwa na kumsababishia mtu tatizo kama la Dimpoz hasa kwa watu wenye maadui na kasumba ya kwenda kupata vinywaji eneo fulani mara kwa mara.
“Ni rahisi sana kufanya jambo kama hilo kwa mhudumu mwenye tamaa ya pesa kwani ni kiasi tu cha kuchukua sumu au kemikali hiyo na kumwekea mteja kwenye glasi ya kinywaji,” alisema Doris Swai ambaye ni mhudumu wa baa moja maarufu iliyopo Kinondoni-Manyanya jijini Dar Ilibainika kwamba, sumu hizo zipo katika makundi ya kemikali za kawaida ambazo ni rahisi kupatikana na mtu kuwekewa kwenye kinywaji bila yeye kujua kutegemeana na mazingira yenyewe ya huduma za vinywaji kwenye viwanja vya starehe kama hotelini, baa, migahawa n.k.
AINA ZA KEMIKALI
Ilifahamika kwamba, aina ya kwanza ya kemikali hizo ni sumu ambazo zina uwezo wa kukwangua au kubabua ndani ya mwili ambazo ni amonia, betri, asidi, dawa ya kusafisha mitaro, magadi-kali inayobabua (caustic soda) pamoja na maji ya magadi-kali yanayobabua (lye). Ilielezwa kuwa, kemikali hizo ni rahisi kupatikana hivyo kufanya jambo hilo kuwa la hatari hasa kwa wale wenye maadui.
DALILI ZA MTU ALIYENYWESHWA KEMIKALI HIZO
Ilielezwa kwamba, dalili za mtu aliyenyweshwa kemikali hizo ni pamoja na kutokwa sana na mate, maumivu mdomoni, kooni, kifuani, tumboni na hata mgongoni, kutapika na shida katika kumeza chakula.
Kwa mujibu wa madaktari wa Dimpoz nchini Kenya na Afrika Kusini, hizo ndizo dalili alizokuwa nazo staa huyo ambapo alikuwa akipata shida kumeza chakula na huenda tatizo hilo likawa lilisababishwa na kemikali ya sumu mojawapo kati ya hizo hapo juu.
Image result for ALIKIBA
DAKTARI SASA
Kwa mujibu wa daktari aliyezungumza na gazeti hili, Dk Godfrey Charles ‘Dk Chale’, sumu za aina hiyo huua taratibu kwani huchukua muda mrefu kubainika na mara nyingi mtu hudhani amepata ugonjwa fulani bila kujua ni sumu aliyonywesha miaka au miezi kadhaa iliyopita. Hata hivyo, baadhi ya wataalam walidai kuwa, endapo mtu atagundua amenyweshwa kemikali hizo ndani ya muda mfupi, ili kumnusuru afya yake kuna taratibu za kufuata za haraka;
Ilielezwa kuwa, mtu aliyenyweshwa mojawapo ya kemikali hizo na kugundua ndani ya muda mfupi hatakiwi atapike bali anaweza kutumia dawa ya mkaa ya kunyonya sumu mwilini (activated charcoal) na kunywa maji mengi kadiri awezavyo kisha atafute wataalam wamtoe sumu hiyo kabla haijaleta madhara.
Hadi sasa Dimpoz hafahamu ni katika mazingira gani alikunywa sumu hiyo kwani kwa akili timamu na kumbukumbu zake hajawahi kutumia sumu ya aina yeyote.
STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Jumamosi
Undani, Ukweli Simu ya Dimpoz..Diamond na Kiba Hatarini
0
September 16, 2018
Tags