Usithubutu Kutoa Mimba...Soma Kisa Hichi cha Ronald na Mama yake

USITHUBUTU KUTOA MIMBA

DOLORES Aveiro ni mama wa staa wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, anaitwa mama wa stadi huyo wa mpira wa miguu kwa kudura za Mungu. Matunda anayokula kupitia mwanaye hakika hakuyastahili. Maana anakula raha alizojaribu kuzihujumu.

Kama mipango ya binadamu peke yake ingekuwa inatosha kutimiza mambo na maazimio, Dolores asingeweza kuwa mwanamke maarufu duniani. Asingeitwa mama wa kijana gwiji wa soka ulimwenguni, anayeichezea Klabu ya Juventus na Timu ya Taifa ya Ureno.

Dolores hakumtaka Ronaldo wakati ikiwa mimba lakini sasa hivi anatamba huku na huko kwamba yeye ndiye mama mzaa nyota. Mungu alimlinda Ronaldo.

Mama huyo, alikusudia hasa kukatisha maisha ya Ronaldo akiwa bado mimba, kwani hata madaktari walipomshauri asifanye hivyo, alitumia mpaka njia za kienyeji.

Dolores ameandika kitabu na kukiita kwa Lugha ya Kireno, Mae Coragem (Mother Courage), maana yake ikiwa ni Ujasiri wa Mama. Ndani ya kitabu hicho Dolores anasema: “Nililenga kutoa mimba ya Ronaldo. Nilitumia njia nyingi bila mafanikio. “Madaktari waligoma kunisaidia kutoa mimba, uamuzi uliofuata baada ya hapo ikawa ni kunywa pombe kali ili kuitoa. Lakini sikupata matokeo niliyohitaji. “Nilitumia kila njia nikashindwa. Sikutaka kumzaa Ronaldo. Sikujua kama atakuja kuwa huyu anayenifanya nijivunie kuwa mama.” Ushuhuda wa mama.

Ronaldo anajua hila za mama yake, na siku moja alimrudi, akamwambia: “Mama angalia, ulitaka kunitoa nikiwa mimba na sasa mimi ndiye kinara wa nyumba yetu. Unanitegemea na familia yetu yote inanitazama mimi. “Tazama jinsi ambavyo dunia inanitazama. Naitwa mchezaji mkubwa duniani. Kila klabu kubwa ya soka duniani ingependa kupata huduma yangu. Unadhani hii ni fahari yangu peke yangu? Inakuhusu na wewe mama yangu. Unapaswa kujivunia sana kuwa na mtoto kama mimi. Usingenipata kama ungefanikiwa kutoa mimba." Hilo no somo kubwa.

Mume wa Dolores, Dinis Aveiro ambaye ni baba wa Ronaldo, alishatangulia mbele za haki kwa maradhi ya kuharibika kwa ini, kutokana matumizi makubwa ya pombe.

Je, Dolores ana uhakika gani? Jinsi Ronaldo anavyofurahia naye mafanikio ya kimaisha, inakuwa ni furaha ya kweli au anamsuta?

Ndimi Luqman MALOTO
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad