Akizungumza jijini Dodoma baada ya mkutano na ukaguzi wa pikipiki ya mfano iliyofungwa tela iliyotengenezwa na Shirika la Mzinga,lililoko chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu, amesema Serikali imedhamiria kuondoa na kukomesha ajali za bodaboda pamoja na kulinda usalama wa watumiaji wa usafiri huo.
Akielzezea juu ya mazungumzo hayo yaliyokutanisha taasisi hizo, Katibu Mkuu Meja Jenerali Jacob Kingu, amesema Wizara yake kwa kushirikiana na wadau wengine kutoka taasisi za serikali; Shirika la Mzinga, Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Kiwanda cha Kutengeneza Magari (NYUMBU) na Jeshi la Polisi watahakikisha wanakuwa na mpango wa pamoja wa kuratibu na kuhakikisha mkakati huo utakaosaidia kupunguza ajali unakamilika.
“Leo tumekutana hapa kujadili jinsi ya kuliendea jambo hili la kufunga tela na kamati ya wataalamu hawa ndio itakutana na kuratibu andiko ambalo litapelekwa kwa viongozi wa wizara mbalimbali zinazohusika na suala la kudhibiti ajali za barabarani na kumlinda mtumiaji wa huduma ya usafiri huo,” alisema Meja Jenerali Kingu.
Aliwaomba wananchi wawe na subira katika kipindi hiki ambacho kamati hiyo ya wataalamu inaenda kuandaa mpango huo, na mapema mwishoni mwa mwaka huu mpango huo utatangazwa .
Akizungumzia pikipiki hiyo ya mfano yenye tela, Mtaalamu kutoka Shirika la Mzinga, Mhandisi Salum Kipande alisema pikipiki hiyo wameitengeneza vizuri na itakua na uwezo wa kubeba abiria wanne na dereva mmoja huku akiahidi kuunga mkono adhma hiyo ya serikali kupunguza ajali za bodaboda nchini kwa kutengeneza pikipiki hizo kwa ustadi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Elimu na Mafunzo wa Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA), Stella Ndimubenya alisema wao kama VETA watahakikisha wanatumia teknolojia waliyonayo kuweka kifaa maalumu ambacho kitadhibiti upakiaji wa abiria kupita kiwango kilichopitishwa na mamlaka husika huku akiahidi kutoa mafunzo kwa madereva pindi pikipiki hizo zitakapopitishwa na kuanza kutumika.