NA ELBOGAST MYALUKO
Katika jitihada za kuendelea kuhakikisha vitendo vya baadhi ya walimu kuchapa hadi kujeruhi au kusababisha vifo kwa wanafunzi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepiga marufuku walimu wa shule za msingi na sekondari kutembea na viboko katika eneo la shule.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe.William Ole Nasha ambapo amewataka walimu kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya utoaji wa adhabu za viboko kwa wanafunzi kulingana na waraka wa elimu wa mwaka 2002 unavyoelekeza.
Ole Nasha ameyasema hayo jijini Mwanza wakati akifungua mafunzo kuhusu uimarishaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa walimu wa ziada 443 wanaofundisha darasa la kwanza na la pili kutoka halmashauri sita za mikoa ya Mwanza na Kagera.
Agizo hilo limetolewa ikiwa ni siku chache baada ya kifo cha mwanafunzi wa darasa la tano shule ya msingi Kibeta Manispaa ya Bukoba, Sperius Eradius, aliyeelezwa kupewa adhabu ya viboko na mwalimu wake wa nidhamu.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu, ADEM, Dkt. Siston Masanja Mgullah, amesema, adhima ya serikali ni kuendelea kuwapatia walimu wengi mafunzo ya ufundishaji wa stadi za KKK. Mafunzo hayo katika kituo cha chuo cha ualimu Butimba yatawahusisha zaidi ya walimu 900 katika awamu mbili.