Yaliyotabiriwa na mbunge wa Ukerewe (Chadema), Joseph Mkundi juu ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere yametimia.
Kivuko hicho kilizama jana katika Ziwa Victoria mita 50 kabla ya kutia nanga huku abiria 44 waliokuwa kwenye kivuko hicho wakifariki dunia hadi zoezi la uokoaji lilipositishwa jana usiku..
Katika moja ya swali alilouliza bungeni hivi karibuni, Mkundi alitaka kupata kauli ya Serikali jinsi itakavyoshughulikia kivuko hicho ili kisije kusababisha maafa.
“Naomba kupata kauli ya Serikali, ni suala ambalo tumekuwa tunalishughulikia mara kwa mara, tuna kivuko kinachounganisha Ukerewe na kisiwa cha Ukara, kivuko hiki kinahudumia watu zaidi ya 50,000.
“Kimekuwa kinaleta shida mara kwa mara na nimekuwa nawasiliana na wizara, sipendi siku moja tuje hapa kuomba rambirambi kwa sababu ya wananchi waliozama katika kivuko kile.” Alisema