Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole amesema kuwa kuna baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani hata wasijisumbue kujiunga na CCM kwani hawatopokelewa na chama hicho.
Akizungumza na www.eatv.tv Polepole amesema kuwa kuna wabunge tayari wameomba kujiunga na CCM na amewakatalia kutokana na tabia zao za kutukana kupitia mitandao ya kijamii.
“Kuna wabunge wameshaomba kujiunga na CCM hasa wa Dar es salaam, lakini kutokana na mienendo yao tumewakataa kwani huwezi tukana maendeleo wakati unatumia hivyo hivyo unavyopingana navyo”, amesema Polepole.
Akizungumzia suala la aliyekuwa Mbunge wa Serengeti (CHADEMA) Marwa Chacha Ryoba amesema kuwa anatakiwa kufuata taratibu zote za chama ikiwa ni pamoja na kufika katika ofisi za CCM wilayani Serengeti ili kukamilisha taratibu zote.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa haki zote na uhuru wa kila mmoja kufanya chochote bila kuvunja sheria ikiwemo kuweka mawazo yako hadharani, tunashukuru Ryoba amesema mwenyewe hadharani kuwa anaomba kujiunga na CCM hivyo afuate taratibu zote akikidhi vigezo sisi hatuna tabu”, amesema Polepole.
Jana usiku Septemba 27, aliyekuwa Mbunge wa Serengeti (Chadema), Marwa Chacha alitangaza kujiuzulu uanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini na kusema kuwa amechukua uamuzi huo kumuunga mkono mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli.
“Wakati nagombea Ubunge niliahidi kuwaletea maendeleo wananchi wangu lakini dhamira yangu haijafanikiwa kutoka na vikwazo ninavyokumbana navyo ndani ya Chadema”, amesema Ryoba.
Chacha Marwa Ryoba anakuwa Mbunge wa sita wa vyama vya upinzani kuhamavyama vyao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi kwa nia ya kuwaletea wananchi maendeleo akiungana na Maulid Mtolea, Mwita Waitara, Julius Kalanga, Godwin Moleli, Zuberi Kachauka ambae anashiriki kampeni za uchaguzi mdogo jimbo hilo la Liwale kwa tiketi ya CCM.