Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage leo Ijumaa Septemba 7, 2018 amejikuta katika wakati mgumu bungeni mjini hapa baada ya kuzomewa na wabunge kutoka Zanzibar.
Alikumbwa na mkasa huo wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Baraza la Wawakilishi (BLW), Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua sababu za Serikali kuendelea kuzuia sukari ya kiwanda cha Mahonda kuuzwa Tanzania Bara.
Katika swali lake, Jaku amesema haiingii akilini kuona bidhaa kutoka Zanzibar kuwa ngumu kuingia katika soko la Tanzania Bara, wakati zile za Tanzania Bara zinaingia kirahisi Zanzibar.
Katika majibu yake, Mwijage amesema katika kipindi cha uongozi wake hawezi kuruhusu sukari kutoka kiwanda cha Mahonda kuletwa Tanzania Bara kwa maelezo kuwa bado kuna vitu vya kuhoji ndani ya kiwanda hicho.
Kauli hiyo ilizua mvutano mkali bungeni na wabunge wa Zanzibar walianza kupiga kelele kwa sauti za juu wakipinga majibu hayo.
“Mheshimiwa mwenyekiti naomba nikuelekeze wewe majibu yangu na wabunge wanaotaka kunisikiliza, lakini wale wasiotaka waache waendelee kupiga kelele tu,” amesema Mwijage.
“Mimi ninasimamia kuwa kiwanda cha Mahonda kinazalisha tani 4,000 wakati mahitaji ya wananchi wa Zanzibar ni tani 20,000, je hiyo wanayotaka kuuza huku wanaitoa wapi? Siko tayari kukubali hata wakizomea.”
Kuhusu sukari iliyorundikana kwenye viwanda, Mwijage amesema vyombo vya dola viko kazini na tayari wamegundua ndani ya uchunguzi huo kuna jinai hivyo kuna watu ambao watashughulikiwa.