Mgombe Ubunge wa jimbo la Ukonga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwita Waitara amesema yeye sio Msaliti bali amechagua CCM ili aweze kumalizia alipoishia hususani swala la barabara , Umeme na Maji katika jimbo hilo.
Waitara aliyasema hayo jana Jumapili Septemba 2 katika Mkutano wake wa Kampuni uliofanyika katika Kata ya kitunda.
Alisema kuhamia kwake CCM ameona imefika mahali kero zinazowasumbua wananchi hataweza kuzitekeleza kwani kuna baadhi ya vikao ukienda ukirudi kwenye vikao vya chama unaambulia matusi.
"Naomba muelewe kwamba mimi nimekulia Kitunda, nimesomea shule Kitunda na nimeoa hapa hivyo najua kero zote zinazowahusu wanakitunda ikiwemo barabara, elimu pamoja na huduma za kijamii kama maji na umeme," alisema.
Hata hivyo, Waitara amesema alipokuwa Chadema ameweza kwenda maeneo yote ikiwemo mitaa 70 kutembelea kina mama vijana wa bodaboda, vikoba hivyo hakuna anayeweza kusimama na kusema kuwa Waitara hajafanya chochote alipokuwa mbunge wa Chadema.
Pia, aliongeza kwa kipindi chote akiwa Chadema ameshindwa kutekeleza baadhi ya changamoto, kwani viongozi wa chama walikuwa wakimwambia afanye hivyo kwa kuwatuakana viongozi wakiwemo mawaziri ambao wengine ni wakubwa kwake jambo ambalo hawezi.
Waitara alisema ilifika mahali kutokana na yaliyokuwa yanaendelea ndani ya Chadema ikiwemo kutoruhusiwa kuhoji mapato na matumizi ya chama.
Kutokana na hilo amesema alikuwa kashafikia hatua ya kuwa mbunge bubu ndani ya Bunge na hivyo hakuona faida ya kuwa mbunge kupitia chama hicho ambacho huruhusiwi hata kuhoji.
Alisema kwa CCM anaona kina faida kwani wabunge wana nafasi katika vikao vyao kukaa na mawaziri wa nchi hii na kuwa na nafasi ya kupenyeza kero za wananchi ili zishughulikiwe.
Mwita amewaahidi wananchi hao kama watamchagua, atazidi kuwaletea maendeleo, kwani aliyafanya hayo akiwa mtoto wa kambo na sasa amerudi nyumbani.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Juu ya CCM Livingstone Lusinde aliwataka watu wa ukonga wasifanye makosa kwani sasa wanachagua Mbunge wa jimbo atakayefanya kazi na serikali na sio uchaguzi Mkuu.
Alisema CCM peke yake ndio inatekeleza ilani Kwa kupewa dhamana ya kuongoza dola hivyo wakichagua mgombea kutoka vyama vingine watakuwa wamejitafutia matatizo wenyewe