SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema uchaguzi mkuu wa Klabu ya Simba utafanyika kwa kufuata mwongozo uliopo katika katiba mpya ya klabu hiyo ambayo imesajiliwa mwaka huu.
Kauli hiyo imekuja baada ya kuwapo kwa sintofahamu ya katiba ipi itakayotumika katika uchaguzi wa klabu hiyo ambao unatarajiwa kufanyika Novemba 3, mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Revocatus Kuuli, alisema katiba hiyo ndiyo inatambulika baada ya kupitishwa na wanachama na baadaye kusajiliwa.
Kuuli alisema wanachama wanatakiwa kuheshimu uamuzi waliopitisha kwenye mkutano na kama kuna malalamiko kuhusiana na uchaguzi huo wanatakiwa kufikisha madai yao katika ngazi husika.
"Uchaguzi utafanyika kwa kufuata katiba ya mwaka 2018, kama kuna mwanachama mwenye dukuduku anatakiwa afuate njia zinazotakiwa kufikisha malalamiko yake, mimi kamati yangu haitasimamia uchaguzi huo, lakini itaufuatilia kutokana na madaraka iliyonayo," Kuuli alisema.
Viongozi wa Simba ambao wako madarakani walimaliza muda wao tangu Juni 30, mwaka huu, lakini sasa uongozi utakaochaguliwa utafanya kazi kwa kushirikiana na wajumbe wa bodi ambao watateuliwa na mwekezaji, Mohamed Dewji, ambaye ana hisa asilimia 49 kwenye klabu hiyo.