Walimu Wanaotuhumiwa Kumpiga Mwanafunzi Hadi Kufa, Washtakiwa kwa Kuua kwa kukusudia

Wanaotuhumiwa kuua mwanafunzi, washtakiwa kuua kwa kukusudia
Chanzo cha walimu wawili wa Shule ya Msingi Kibeta kufunguliwa kesi ya mauaji ya kukusudia ni mwanafunzi Sperius Eradius kupiga kelele akiomba msaada huku kipande cha kuni kikitumika kama mbadala wa fimbo.

Watuhumiwa hao Respicius Mtazangira na Julieth Gerald wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Bukoba leo Septemba 3, 2018 na kusomewa shitaka la mauaji huku kesi ikiahirishwa hadi Septemba 17.

Akihojiwa na Mwananchi kuhusu sababu za watuhumiwa kufunguliwa shitaka la mauaji ya kukusudia, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Athumani Matuma amesema kipande cha kuni ndicho kilitumika kumwadhibu marehemu huku akipiga kelele za kuomba msaada kwa wenzake.

Katika kesi hiyo namba 18/2018, Wakili Matuma ameieleza mahakama hiyo upelelezi umekamilika na Hakimu Mkazi Mfawidhi, John Kapokolo akisema mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji na watuhumiwa kupelekwa rumande.

Wakili huyo amesema ofisi yake inafanya taratibu za kuhamishia kesi hiyo Mahakama Kuu kwa ajili ya kupangiwa tarehe za kuanza kusikilizwa kwa kuwa upelelezi tayari umekamilika.

Kifo cha mwanafunzi Sperius Eradius kilionekana kugusa hisia za watu wengi kutokana na mazingira yake ambapo marehemu alidaiwa kuiba mkoba wa mtuhumiwa wa pili Julieth Gerald na kudaiwa kumpeleka mwanafunzi huyo kwa Respicius anayesimamia nidhamu.

Pia, kifo hicho kiliibua mgogoro kati ya Serikali na familia ya marehemu ambayo iliomba ufanyike uchunguzi huru baada ya kutoridhika na ripoti ya awali ya daktari iliyoonyesha mwanafunzi huyo kuwa na makovu ya siku zilizopita.

Serikali ilikubaliana na ombi la familia na baada ya uchunguzi wa pili mwili wa marehemu ulizikwa wilayani Muleba na kuhudhuriwa na Naibu Waziri Tamisemi, John Kandege na kutoa ubani wa Sh2 milioni.

Pia, kufuatia tukio hilo, Serikali imechukua hatua kadhaa ikiwamo kuusimamisha uongozi wa shule na kuunda tume ya kuwachunguza kama walikuwa wanasimamia majukumu yao ipasavyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad