Wanaoziponda Bomberdier' Dreamliner Kukiona

Wanaoziponda Bomberdier' Dreamliner Kukiona
Pamoja na Rais Dk John Pombe Magufuli kufanya jitihada nyingi katika kuhakikisha tunafikia kiwango cha juu kama nchi za wenzetu katika usafiri wa anga, lakini bado kuna baadhi ya Watanzania ambao siyo wazalendo na nchi yao, wanatafuta kila njia kutia dosari Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Leo kwenye safu hii tunakuletea mahojiano kati ya Mwandishi Wetu, Shamuma Awadh na Msemaji wa Shirika la Ndege la Tanzania, Josephat Kagirwa ambaye amefunguka mambo mengi ambayo huenda ulikuwa huyajui au ulikuwa unapata utata, fuatana naye katika mahojiano hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita ili uwe balozi wa kueneza uzuri wa shirika letu la ndege nchini;

Mwandishi: Historia ya shirika hili ikoje kwa ufupi?

Kagirwa: Air Tanzania ilianzishwa mwaka 1977 ikiwa ni shirika la ndege ila kutokana na changamoto za hapa na pale mpaka kufikia mwaka 2002 ndipo ilibadilika rasmi kuwa kampuni ya Serikali ingawa lilikuwa linaendeshwa likiwa dhaifu sana ndipo mwaka 2016, Serikali ya awamu ya tano ikaamua kuifufua tena rasmi na ndiyo mpaka sasa tumefika hapa.
Image result for dreamliner tanzania
Mwandishi: Ushindani ukoje na makampuni binafsi?

Kagirwa: Ushindani ulikuwa mkubwa sana mwanzoni ila kwa sasa siyo sana kwa sababu tuna ndege kubwa na zenye ubora, ndege zetu zinachukua muda mfupi sana angani, hazina kelele na pia sisi ndiyo pekee tunatoa madaraja mawili yaani Business Class na Economic Class ambayo ni tofauti na wengine, kwa hiyo tumeboresha vitu ambavyo vinatufanya tuendane na ushindani uliopo sasa.

Mwandishi: Mmejizatiti vipi kuhakikisha usalama wa wateja wenu?

Kagirwa: Usalama wa wateja wetu tumefanya ni kipaumbele sana hata kwenye ‘vision’ (maono) ya kampuni, walinzi wapo vizuri kuhakikisha tunadhibiti vibaka na watu hatari wanaohatarisha maisha ya wateja wakiwa uwanja wa ndege, kwa hiyo ulinzi unazingatiwa kwa kiwango cha hali ya juu sana. Vilevile ndege zetu zipo chini ya uangalizi mkali wenye umakini na ‘service’ hufanywa mara kwa mara.

Mwandishi: Vipi kuhusu bei zenu, zimeangalia hali ya sasa ya wananchi?

Kagirwa: Bei zetu ni nafuu sana maana bei ni za kawaida, tofauti na makampuni mengine, zinaendana sawa na hali ya wananchi na pia hali halisi ya soko yaani siyo ya kutufanya tufe, ni ya kiwango ambacho hata sisi kama kampuni tutaweza kujiendeleza kibiashara. Lakini pia tumeweka bei katika mgawanyo tofauti ili wanaowahi kukata tiketi wapate kwa bei ya chini.
Image result for dreamliner tanzania
Mwandishi: Kwa nini mwanzo kampuni ilikwama?

Kagirwa: Haikukwama ila ilikuwa inaendeshwa kwa udhaifu sana na ndiyo maana Serikali ya awamu ya tano ikaamua kuifufua na ni mikakati ambayo ilikuwepo katika ilani ya chama ya mwaka 2015. Vitu vingi ambavyo vimeboreshwa ikiwemo kununua ndege zetu wenyewe, kitu ambacho kilikuwa kinaonekana kama hakiwezekani, lakini tumeweza na tunajivunia.

Mwandishi: Ni mafanikio yapi ambayo mmeyapata mpaka sasa?

Kagirwa: Kwanza tumeweza kununua ndege tatu za kwanza aina ya Bombadier Q4100 baadaye tukaongeza tena nne ambazo zinaitwa Airbus 220-3100 mbili nyingine ni Boing 787- 800 Dreamliner. Katika zote hizo nne zimeshawasili na tunategemea mwezi wa kumi na moja ziwasili airbus mbili na mwaka kesho Dreamliner moja. Tangu zimefika tumeshatua katika viwanja kumi na moja hapa ndani ambavyo ni Zanzibar, Kilimanjaro, Mwanza, Bukoba, Kigoma, Tabora, Dodoma, Mbeya, Songea, Mtwara na Dar es Salaam na vingine vitatu vya nje ya nchi ambavyo ni Comoro, Entebbe na Bunjumbura. Pia tumeongeza miruko kwani kuna baadhi ya mikoa tunaenda mara mbili kwa siku na mingine ni kila siku. Vilevile tumeongeza abiria kabla ya Oktoba 2016 tulikuwa tunabeba abiria pungufu ya 5,000 sasa hivi tunabeba abiria zaidi ya 21,000. Na kwa upande wa mapato, mwanzo ilikuwa shilingi milioni mia saba kwa mwezi sasa hivi ni shilingi bilioni nne kwa mwezi.
Image result for dreamliner tanzania
Mwandishi: Je, kuna marubani ambao mmewaajiri na elimu yao wamechukulia Tanzania?

Kagirwa: Hapana kwa sababu kwanza hatuna vyuo vya urubani hapa nchini vyenye kutoa elimu yenye umahiri. Lakini marubani tulionao wamesoma nje ila ni Watanzania.

Mwandishi: Mnasapoti vipi elimu kwa wenye ndoto za urubani?

Kagirwa: Namna tunavyowasapoti ndoto, kuna mipango ya kuanzisha vyuo vitakavyowafundisha kwa sababu elimu ya nje ni ghali sana, inafikia hadi shilingi milioni mia moja. Pia tunahimiza watu wakasome NIT ikiwa ni chuo pekee ambacho kitatoa elimu hiyo hapa nchini hivi karibuni na ada yake itakuwa nafuu kiasi cha shilingi milioni 30 tu.

Mwandishi: Mmejipanga vipi kutoa elimu kwa jamii ya watu ambao wanadhana potofu na kampuni hii ya ndege?

Kagirwa: Tunaelimisha wananchi kwa kufanya matangazo kwenye redio na runinga na mitandaoni kwa kuandika vitu vyenye kuelimisha jamii ili ipate uelewa na isishike vitu vyenye kupotosha kwa urahisi na hata ile dhana potofu ya sisi ni wachelewaji sasa hivi tunaondoka kwa wakati, na siku hizi ‘hatu-cancel’ (kufuta) safari hovyohovyo kwa sababu ndege zipo nyingi au tukishindwa tunawapeleka katika ndege nyingine endapo ikitokea dharura. Kutokana na kufanya hivyo, watu wanaanza kuwa na imani na sisi.

Mwandishi: Ni jitihada zipi zinafanyika kukabiliana na watu ambao wanaichafua kampuni hii kwa mambo ya uongo na kupotosha?

Kagirwa: Sheria zipo na zitafuata mkondo wake ili kukomesha tabia hiyo maana wanaharibu kampuni na sisi hatuwezi kuvumilia kwa sababu Rais wetu wa nchi anajitahidi kuiinua hii kampuni halafu mtu au watu wanaamua tu kutaka turudi tulikotoka, hatuwezi kufumbia macho, lazima wanaoziponda ndege zetu watakiona kwa kuwajibishwa na sheria.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad