Rais Yoweri Museveni mwishoni mwa wiki iliyopita alizomewa na watu alipotembelea eneo ambalo aliyekuwa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Buyende, Muhammad Kirumira aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Wakazi wa eneo hilo waliokuwa wamekusanyika mahali alipouawa Kamanda huyo walimzomea Museveni wakimwambia wamechoshwa na mauaji yanayoshuhudiwa katika nchi hiyo.
“Tumekuchoka wewe pamoja na watu wako wanaovaa sare (askari). Tunakutaka uchukue hatua. Watu wanakwisha, utatawala nini, nchi isiyo na watu?” alisema kwa sauti mtu mmoja kutoka katikati ya umati wa watu.
Maofisa wa jeshi walianza kutawanya watu hao wenye hasira na wakawaamuru waandishi wa habari kutorusha tukio hilo mubashara. Watu walilalamika kwamba kabla ya kuuawa kwake, Kamnda Kirumira na baba yake Abubaker Kawooya waliomba ulinzi kutoka kwa Rais wakihofia maisha yao.
Watu wenye silaha wakitumia usafiri wa bodaboda walimpiga risasi Kamanda Kirumira pamoja na mkewe Mukyala Ali ambaye alikuwa na kibanda cha kubadilishia fedha katikatika ya eneo la kibiashara la Bulenga. Wawili hao ambao walikuwa ndani ya gari yao iliripotiwa waliuawa karibu na nyumbani kwao Bulenga, wilaya ya Wakiso.
Katika hatua nyingine, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Emilian Kayima alifukuzwa na wananchi alipokwenda kushiriki maziko ya Kamanda Kirumira Jumamosi iliyopita.
Wengine waliokuwa na wakati mgumu ni Waziri Jeje Odongo ambaye alirushiwa mawe wakati msemaji wa polisi alishambuliwa.
Waombolezaji waliswalia mwili wa Kirumira katika Msikiti wa Old Kampala kabla ya kupelekwa makaburini. Waombolezaji wenye hasira nao walikuwa wakiimba nyumbani kwake Bulenga.
Wakati fulani walisikika wakiimba ‘Nguvu ya umma – nguvu yetu.’ Hiyo ni kaulimbiu ambayo huwa inatumiwa na mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.