Watanzania 27 wamekamatwa mjini Mombasa Kenya baada ya kuingia nchini humo bila vibali maalum.
Mamlaka ya usalama huko Mombasa inaendelea na mipango ya kuwarejesha nchini kwao.
Baadhi ya watu hao wameshikiliwa na polisi katika kituo cha Likoni wakati wakisubiri kurejeshwa nyumbani.
Kamanda wa polisi wa Mombasa Johston Ipara ameeleza kwamba Watanzania hao ni miongoni mwa wahamiaji wengine kutoka Congo, Somalia, Eritrea na Ethiopia ambao walikamatwa kwa kutokuwa na vibali vya kusafiria.
Ingawa watu wa Afrika Mashariki huwa wanaweza kutumia kitambulisho cha taifa kuweza kuingia na kutoka katika nchi zote tano za Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na Kenya, Burundi ,Rwanda,Tanzania na Uganda.
Kamanda Ipara alisema watu hao hawakuwa na hata vitambulisho vya taifa.
Raia hao walikamatwa katika ukaguzi ambao umekuwa ukifanyika katika nchi nzima.
Hata hivyo ilionekana kuwa hapakuwa na muongozo mzuri katika ukaguzi huo na hatua zilizochukuliwa na polisi na utawala.
Siku ya Jumatano ,baadhi ya wageni katika nchi hiyo walipelekwa mahakamani lakini kesi yao ikafutiliwa mbali .
Wakili wa serikali Henry Nyakweba aliiambia mahakama kuwa watapitia upya mashtaka ya watu hao kuwepo nchini Kenya bila kibali.
Tangu mwezi wa tano serikali ya Kenya ilianza udhibiti kwa wageni wasiokuwa na vibali haswa wale wanaofanya kazi nchini humo.