Watu sita Wameripotiwa Kufariki kwenye ajali ya MV Nyerere Mpaka Sasa


Pichani kikosi cha uokoaji kikiendelea na zoezi la uokoaji abiria waliozama kwenye MV Nyerere.

Watu sita wamefariki dunia na wengine 20 kuokolewa baada ya Kivuko cha MV Nyerere  mkoani Mwanza kinachofanya safari kati Bugorora katika Kisiwa cha Ukerewe na Kisiwa cha Ukara katika Ziwa Victoria kuzama leo Alhamis Septemba 20,2018 mchana katika ziwa Victoria.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, George Nyamaha amesema timu ya uokoaji bado inaendelea na kazi ya uokozi na kuna uwezekano idadi ya waliofariki dunia ikaongezeka.

“Kuna maelezo kuwa katika kivuko hicho kulikuwa na abiria zaidi ya 100 baada ya kupinduka idadi kubwa ya watu wanahofiwa kufariki dunia,” amesema Nyamaha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shana amesema kivuko hicho kimezama wakati kikielekea katika Kisiwa cha Ukara.

Kamanda Shana amesema kuwa kivuko hicho kimezama leo mchana baada ya kupinduka. “Kiliondoka saa 6 mchana na ilipofika saa nane kamili mchana kilipinduka,” amesema.

 Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Hassan Karonda amekiri kuzama kwa kivuko hicho Kivuko hicho cha Mv Nyerere kina uwezo wa kubeba abiria 100, tani 25 za mizigo na magari madogo matatu.

Mwezi Julai kivuko hicho kilifungwa injini mpya baada ya awali kupata hitilafu na kimekuwa kikitoa huduma kwa watu wa Ukerewe tangu 2004
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad