Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waishio nje ya nchi wajiepushe na vitendo vya uhalifu hasa biashara ya dawa za kulevya ambayo inachafua jina na heshima ya nchi kimataifa.
Majaliwa ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo Septemba 3, 2018, kwenye ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini China uliopo jijini Beijing wakati akizungumza na Watanzania waishio humo.
“Nawasihi wote mnaoishi nje muachane kabisa na biashara haramu ya dawa za kulevya kwa sababu inalitia doa Taifa na adhabu yake katika baadhi ya nchi ni kifo pia tukumbuke Tanzania ni nchi nzuri na inaheshimika duniani kwahiyo tuilinde heshima hiyo,” alisema.
Mbali na hilo Majaliwa pia amewataka Watanzania waishio nje ya nchi wahakikishe wanashiriki kikamilifu kujenga uchumi wa nchi yao kwa kushawishi wawekezaji wenye mitaji mikubwa waje kuwekeza nchini na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania.
Miaka ya hivi karibuni imekuwa ikiripotiwa biashara ya dawa za kulevya kuhusisha watanzania ambao mara nyingi huwa wanakumbana na adhabu za mataifa hayo ikiwemo kufungwa maisha, kunyongwa na muda mwingne kifo.