Zifahamu Dalili za mtu Anayetaka Kujiua



Maisha ya mwanadamu yanapitia changamoto nyingi sana hadi kufikia kilele cha mafanikio, changamoto hizo zinaweza kumfanya mwanadamu kukata tamaa na wakati mwingine kufikiria maamuzi magumu ya kujitoa uhai wake.


Ugumu wa maisha, mkanganyiko wa kifamilia na mahusiano ya kimapenzi ni kati ya sababu nyingi zinazosababisha mtu kuchukua uamuzi huo mgumu.

Je! utamgundua vipi mtu mwenye dalili za kutaka kujiua?, kupitia kipindi cha SUPA MIX kinachorushwa na East Africa Radio, Mwanasaikolojia na mhadhiri wa chuo kikuu, Novelt Deogratius amezitaja baadhi ya dalili za kumgundua mtu wa aina hiyo ambapo amesema,

“ Dalili kuu ambazo unaweza kumgundua mtu anayetaka kujiua ni, kwanza kabisa kujitenga sana na watu, mtu kama huyu anapenda sana kukaa peke yake japo kwenye hili sio wote wanaopenda kujitenga wana hatari ya kufikia maamuzi hayo magumu. Kiashiria kingine ni mtu kulizungumzia sana suala la kujiua, mfano mtu hutumia maneno kama ‘natamani kujiua, au mkiskia nimekufa msishangae’ ”.

Dalili nyingine aliyoitaja mwanasaikolojia huyo ni mtu kuandaa mazingira rahisi ya yeye kujiua, ambapo amesema mtu kama huyo hupenda kujiwekea mazingira yake vizuri kama vile kununua sumu, kamba na kuandika waraka wa mwisho atakaouacha baada ya kujiua, japo maandalizi hayo hufanya kwa siri kiasi cha kwamba ni vigumu kuweza kumtambua.

Novelt Deogratius pia amesema kuwa wanaume ndiyo wanaoongoza kwa kujiua kutokana na kutopenda kuweka wazi sana matatizo na changamoto zao huku wanawake wakiwa wanaongoza kufanya majaribio mengi ya kujiua ambayo hayafanikiwi.

Kwa upande wa makundi ya kijamii, vijana kati ya umri wa miaka (15-29) ndiyo wanaoongoza kujiua kwa nchi za kiafrika huku kundi la wazee likiongoza katika nchi zilizoendelea kutokana na muda mwingi kuishi wakiwa peke yao bila kuzungukwa na ndugu na watu wao wa karibu tofauti na wazee wa bara la Afrika ambao katika umri wao wanaangaliwa sana na watoto wao, ndugu na jamaa.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Afya duninai (WHO), takribani watu 800,000 wanakufa kwa kujiua duniani kila mwaka huku wengine wengi wakifanya majaribio kadhaa. Asilimia 79 ya vifo hivyo vitokanavyo na watu kujiua hutokea katika nchi zenye uchumi wa chini na zenye uchumi wa kati.

Mwanasaikolojia huyo ametoa ushauri kwa jamii kujihusisha sana na kumcha Mungu na kuwaona wataalamu wa kisaikolojia inapobidi, ikiwa ni njia sahihi ya kuzuia kutokea kwa tatizo hilo kwa kiasi kikubwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad