Abiria waliokuwa wakisafiri kupitia shirika la ndege la Afrika Kusini SA 286 wakitokea Johannesburg wakielekea Hong Kong wamejikuta wakipata adha ya kupekuliwa baada ya kutua, kufuatia baadhi yao kudai kuibiwa mali zao za thamani angani zikiwemo fedha na saa.
Kwa mujibu wa mzungumzaji wa SAA, Tlali Tlali amethibitisha kutokea kwa tukio hilo siku ya Jumatatu wakati wakiwa safarini kuelekea Hong Kong.
“Abiria wawili wamewalalamikia watumishi wetu wakidai kupoteza mali zao za thamani (fedha na saa),” amesema Tlali.
Tlali ameongeza “Baadhi ya walalamikaji wameweza kuwataja baadhi ya abiria ambao wamewashuku kufanya kitendo hicho baada ya kuwaona wakifanya upekuza wakati wengine wakiwa wamelala.”
Hata hivyo mara baada ya kutua kwenye jiji la Hong Kong abiria wote walilazimika kupekuliwa ili kuhakikisha vitu hivyo kupatikana na hatimaye saa na fedha kukutwa zimefichwa licha ya kuwa hakuna aliyekamatwa katika tukio hilo.