Mfanyakazi wa mgahawa mmoja katika mji wa New York nchini Marekani amefukuzwa kazi kufuatia video iliyosambaa mtandaoni iliyomuonesha akimmwagia maji raia mmoja asiye na makazi aliyekuja katika mgahawa huo.
Raia huyo aliyejulikana kwa jina la Jeremy Young alikuja katika mgahawa huo unaouza vyakula vya ngano na kahawa kwaajili ya kuchaji simu yake ili aweze kuzungumza na mama yake ndipo alipopitiwa na usingizi.
Baada ya muda kupita ndipo mfanyakazi huyo alipokuja na kummwagia maji akimtuhumu kwa kuwasumbua wateja wake wanaokuja kila siku kupata mahitaji muda huo huku ajikijichukua video ambayo imesambaa mtandaoni.
Tukio hilo likawalazimisha wamiliki wa mgahawa kutoa taarifa rasmi ya kumfuta kazi na kuahidi kumuomba radhi muathirika wa tukio hilo.
" Mfanyakazi aliyejihusisha na tukio hili ameshafukuzwa kazi na tunafanya jitihada za kumpata muathirika wa tukio ili tuweze kumuomba msamaha ", imesema taarifa hiyo.
" Ninamshangaa mfanyakazi huyu alikuwa na sababu gani ya kufanya tukio hili, kijana wangu ni mkarimu, mpole, hamsumbui mtu na haongei na mtu hadi atakapoongeleshwa ", amesema Betty Jo Craven ambaye shangazi wa Young.
Jitihada za kumchangia kijana huyo kupitia mtandao zimeweza kuzaa matunda kwa kifikisha kiasi cha dola 7,700 ambazo ni sawa na Shilingi 17.5 millioni za kitanzania.