Dar es Salaam. Hotuba ya dakika 15 ya Rais wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi aliyoitoa Ikulu jijini Dar es Salam leo Jumatano Oktoba 3, 2018 imemtoa machozi mkuu wa Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza.
Mwinyi ambaye ni mdhamini wa Skauti nchini alipewa nafasi ya kuzungumza baada ya Rais John Magufuli kuwaapisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Faraji Mnyepe na Mahiza.
Katika hotuba yake, Mwinyi amezungumzia mambo mbalimbali ikiwamo kuwataka Skauti wafanye kazi kwa kufuata kanuni ili wasimtie aibu yeye na Rais Magufuli ambaye alimteua kushika nafasi ya udhamini wa skauti.
“Leo nina miaka karibu 94, sina siku nyingi za kuiacha dunia, sitaki niende huko ninakokwenda na aibu nyuma yangu,” amesema Mwinyi, maneno yaliyomfanya Mahiza kuinama na kufuta machozi.
Mwinyi aliendelea na hotuba yake ya dakika 15 na kueleza namna anavyomhusudu Rais Magufuli kwa mambo makubwa ambayo anayafanya kwa maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake Rais Magufuli amesema Mwinyi ni moja ya viongozi wanyenyekevu tofauti na wengine hasa waliowahi kushika madaraka makubwa. Amesema atazidi kumwombea aishi zaidi ili aendelee kutumika katika maendeleo ya nchi.
“Ni mzee mmoja wapo ambaye ni mnyenyekevu sana, hana makuu, anajishusha, anatambua kuna kuishi na kuna kufa. Mmemsikia amezungumza mwenyewe, anataka akumbukwe kwa mazuri anayoyafanya, ni watu wachache sana ambao wanakumbuka haya,” amesema Rais Magufuli.