HIVI karibuni kijana mmoja wa Indonesia aliokolewa baharini baada ya kupotea huko kwa muda wa siku 49 akiwa katika mtumbwi wake wa kuvulia samaki. Lakini cha kustaajabisha, Aldi Novel Adilang aliliambia shirika la habari la utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa hiyo haikuwa mara yake ya kwanza kuokolewa baharini.
Adilang mwenye umri wa miaka 18 amewahi kuokolewa kwa namna ya kushangazam si mara moja peke yake bali mara tatu. Ingawa wakati huu habari ya kupotea kwake imeweza kufahamika zaidi duniani kwa sababu alikuwa katika eneo la mbali.
Kijana huyo aliyekuwa anafanya kazi ya kuvua katika mtumbwi wake wenye muonekano wa kibanda, ulionekana ukielea katikati ya bahari huku ukiwa umefungwa kamba. Tarehe 14 Julai, Adilang alikuwa ameufunga kamba kilomita 125 pembezoni mwa ufukwe wa bahari ili aweze kuuona wakati anavua.
Adilang anasema mtumbwi uliharibika baada ya rafiki yake kuukarabati. Anasema hakufahamu wakati ambao alipoteza uelekeo.
“Nilikuwa nimelala hivyo sikujua kama nilikuwa napoteza uelekeo, siku chache za mwanzo, chakula nilichokuwa nimebeba kwnye chombo changu kilinisaidia lakini kiliisha ndani ya wiki moja tu.
“Hivyo mchele, maji safi, viungo na vitu vingine viliisha. Ili niweze kuendelea kuishi ilinibidi niwe navua samaki na kuchoma sehemu ya mtumbwi wangu ili kupata moto wa kupikia na niliwahi kula hata samaki bila kumpika”.
Changamoto nyingine ambayo alikutana nayo ilikuwa ni kupata maji safi. Hivyo katika kutafuta suluhisho la jambo hilo alizilowesha nguo zake na kunywa maji ya baharini kwa kutumia nguo kwa madai kuwa nguo yake ilikuwa inachuja maji kuwa safi na kupunguza ladha ya chumvi ya maji ya bahari.
Katika siku 49 akiwa anaelea katika maji, zaidi ya meli 10 zilipita katika eneo alilokuepo na hakuna iliyemuona.
“Nikiwa peke yangu katikati ya bahari niliimba nyimbo za dini na kusoma Biblia ambayo nilikuwa nimeibeba huku nikiendelea kusali, nikiwa na matumaini ya kuwaona wazazi wangu tena,” anasema.
Aidha, kijana huyo alikiri kuwa kuna wakati alipatwa na msongo wa mawazo na alitamani kujizamisha mwenyewe baharini lakini maombi aliyokuwa anayafanya yalimpa nguvu ya kuwa na matumaini ya kuokolewa.
“Tarehe 31 Agosti, niliiona meli iliyokuwa imebeba nishati za kupikia. Wakati huo nilikuwa ninalia na kusema nisaidie, nisaidie, yaani hicho ndicho kitu pekee nilichokuwa nakifahamu kwa wakati huo na kwa bahati nzuri wafanyakazi wa meli hiyo waliniona na kuniokoa. Kitu cha kwanza walichofanya baada ya kuniokoa ni kunipa maji na kunibadilisha nguo,” anaendelea kusema.
Adilang anasema alikaa kwenye meli hiyo kwa muda wa wiki moja mpaka ilipofika mwisho wa safari nchini Japan. Alipowasili Japan tarehe 6 Septemba alirudi kwao Indonesia baada ya siku mbili na kujumuika na familia yake
Adilang anasema mara mbili alizokwama baharini zilimchukua muda mfupi. Mara ya kwanza ilichukua wiki moja na kusaidiwa na mmiliki wa boti ambapo mara ya pili ilichukua siku mbili na pia alipata msaada kutoka kwa mmiliki wa boti.
Akiwa katika chombo chake cha kuvulia hakuwa na vitendea kazi vyovyote vya kuonyesha ishara ya anakoelekea zaidi ya tochi ambayo ilikuwa imebuniwa kuwavutia samaki. Kila wiki kijana huyu alikuwa anavua samaki ambao walichukuliwa na kampuni aliyokuwa anafanyia kazi.
Adilang alikuwa katika mkataba wa mwaka mmoja ambapo alikuwa analipwa dola 134 kila mwezi Lakini baada ya tukio hili amehaidi hatakwenda tena kuvua.