Bahari mbalimbali duniani ziko hatarini kuwa na uchafu wa plastiki zaidi ya idadi ya samaki kufikia mwaka 2050, kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Ellen MacArthur Foundation.
Foundation hiyo iliyoanzishwa na Ellen mwaka 2010 baada ya kufanya utafiti duniani kote kuhusu namna ya kuboresha mazingira imeeleza kuwa takribani tani bilioni 8.3 za plastiki zimezalishwa tangu mwaka 1950, ambapo 60% ya plastiki hizo zimeishia kwenye ardhi au mazingira asilia.
Kutokana na hali hiyo, Ellen MacArthur Foundation imefanikiwa kushawishi makampuni makubwa yanazalisha plastiki, serikali pamoja na taasisi kadhaa zisizo za kiserikali kuungana na kampeni ya marafiki wa mazingira.
“Inatia moyo kuona kwamba makampuni mengi na Serikali wanasikiliza hitaji la umma la kukomesha uchafu wa plastiki na wameahidi kuchukua hatua kwa vitendo. Hatua hii inapaswa kuchukuliwa duniani kote,” Julian Kirby ambaye anaongoza kampeni hii anakaririwa na BBC.
Kwa mujibu wa Ellen MacArthur Foundation, makampuni yanayoongoza kwa uzalishaji wa chupa za plastiki kama Coca-Cola, H&M na L’Oreal yameahidi kwa kusaini makubalino ya kuchukua hatua za kutokomeza uchafu wa plastiki kufikia mwaka 2025.
Akieleza hatua zilizoahidiwa na makampuni hayo, amesema ni pamoja ana kuhakikisha chupa za plastiki zinaweza kutumika zaidi ya mara moja, kutengeneza chupa/bidhaa za plastiki ambazo ni rahisi kurejeshwa na kutengeneza upya bidhaa (recycled) ili kuongeza idadi ya plastiki zinazoweza kutumika upya baada ya matumizi badala ya kutupwa.