Klabu ya soka ya Barcelona kupitia kwa makamu wake wa Rais, Jordi Cardoner, imeweka wazi kuwa kwasasa haina mpango wa kumnunua tena mchezaji wake wa zamani Neymar Jr ambaye alitimkia PSG msimu uliopita.
Akiongea na Radio moja huko Catalunya, Cardoner, amesema hakuna mazungumzo ya ndani yanayofanyika kuhusu uwezekano wa kujaribu kumsajili tena Neymar.
''Ikiwa tulitaka kumsaini basi bodi itahitaji kujadili lakini kwasasa hakuna mtu aliyesema juu ya hilo kwenye bodi. Yeye ndiye aliyeondoka lakini kurudi sio tatizo na kama itahitajika hivyo basi mazungumzo yatafanyika lakini kwasasa hakuna aliyeongea naye'', amesema.
Ripoti nchini Hispania wiki hii zimeeleza kuwa Barca ina nia ya kumerudisha Camp Nou nyota huyo raia wa Brazil mwenye miaka 26, ikiwa ni miezi 14 tangu ajiunge na mabingwa wa Ligue 1 kwa dau la rekodi ya dunia € 222million, zaidi ya shilingi bilioni 600.
Tayari Neymar amefunga mabao 8 na kusaidia mengine matatu kwenye mechi 9 za msimu huu akiiwezesha timu yake kuongoza ligi ikiwa na alama 27.